2016-08-07 10:16:00

Wasomi kuwasha moto wa hekima na maarifa wakati wa Jubilei yao!


Maarifa na huruma ya Mungu ndiyo tema itakayoongoza maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kwa vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu kutoka sehemu mbali mbali za dunia hapa Roma kuanzia tarehe 7- 11 Septemba 2016. Zaidi ya wawezeshaji 300, washiriki 1000 na vipindi 20 vitatumika katika kuchambua na kupembua kwa kina na mapana masuala ya kiuchumi, mawasiliano ya jamii, taalimungu, saikolojia, fedha pamoja na kuwa na majadiliano na wawezeshaji ili kuzama zaidi katika tema hizi. Mwishoni, wajumbe watapata fursa ya kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko.

Maadhimisho haya yameandaliwa na Baraza la Kipapa la Elimu Katoliki kwa ushirikiano na Idara ya Utume kwa Vyuo vikuu, Jimbo kuu la Roma pamoja na Wizara ya elimu, Vyuo Vikuu na Tafiti nchini Italia. Askofu msaidizi Lorenzo Leuzzi anayeshughulikia kwa karibu zaidi utume wa wanafunzi vyuo vikuu Jimbo kuu la Roma anasema, maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kwa wasomi ni muhimu sana ili kuweza kukita ufahamu na huruma katika utekelezaji wa mikakati mbali mbali ya maisha. Changamoto kubwa iliyoko mbele ya walimwengu ni kujenga utamaduni wa kushirikiana na wote kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya binadamu sanjari na kukabiliana na changamoto za maisha.

Vyuo vikuu pamoja na taasisi za elimu ya juu zina mchango mkubwa katika maisha ya binadamu: kiroho na kimwili. Maadhimisho haya yatazinguliwa rasmi hapo tarehe 7 Septemba 2016 kwenye Chuo kikuu cha Kipapa cha Laterano kwa uwepo na ushiriki wa wasomi Claude Cohen – Tannoudji na Peter Van Inwagen. Siku hii itafungwa rasmi kwa Masifu ya Jioni yatakayongozwa na Kardinali Peter Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa la haki na amani.

Tarehe 8 Septemba 2016 maadhimisho haya yatafanyika katika vyuo vikuu vilivyoko hapa mjini Roma sanjari na Jukwaa kuhusu tafiti, wafanyakazi katika vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu na mwishoni ni vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu. Jioni kutafanyika tamasha la muziki na Kardinali Gianfranco Ravasi, Rais wa Baraza la Kipapa la Utamaduni atatoa tafakari.

Tarehe 9 Septemba 2016 wajumbe wataoneshwa ramani ya Mji wa Roma na baadaye jioni watashiriki katika Ibada ya Misa takatifu kwa ajili ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu itakayoongozwa na Kardinali Giuseppe Versaldi, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Elimu Katoliki. Jumamosi tarehe 10 Septemba, washiriki watakutana na Baba Mtakatifu Francisko kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Askofu msaidizi Lorenzo Leuzzi anakaza kusema, kufahamu maana yake ni kuwa na huruma, ili kushiriki katika mchakato wa ujenzi wa matumaini ya leo na kesho iliyo bora kwa vijana wa kizazi kipya na wala si tu kuwajaza ujuzi na maarifa, bali kuwaunda barabara! Wadau kutoka vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu wanakutana katika ulimwengu wa elimu ya huruma ya Mungu kama zawadi na wala si haki. Elimu inayoiwezesha Jamii kuwa na matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi kwani maendeleo mapya ni jambo linalowezekana.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.