2016-08-06 08:53:00

Mwaka wa neema na huruma ya Mungu!


Baba Mtakatifu Francisko tarehe 4 Septemba 2016 majira ya saa 4:30 asubuhi kwa Saa za Ulaya anatarajiwa kuongoza Ibada ya Misa Takatifu kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican na kumtangaza Mwenyeheri Mama Theresa wa Calcutta kuwa Mtakatifu, wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Mama Theresa wa Calcutta (1910- 1997) anakumbukwa na wengi kutokana na majitoleo yake kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Huyu alikuwa ni Mwanamke wa shoka alithubutu kusimama kidete kulinda na kutetea Injili ya uhai, utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, mwaliko kwa waamini pamoja na watu wenye mapenzi mema kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu katika maisha yao. Kwa hakika mwaka 2016 ni mwaka wa neema na huruma ya Mungu. Tukio la kutangazwa kwa Mama Theresa kuwa Mtakatifu lina maana ya pekee kabisa kwa familia ya Mungu nchini Kosovo na Albania katika ujumla wake.

Katika mkesha wa Ibada ya kumtangaza Mama Theresa wa Calcutta kuwa Mtakatifu kutafanyika tamasha la Muziki kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Paulo njea ya kuta mjini Roma, lililoandaliwa na familia ya Mungu kutoka Kosovo inayotaka kushirikisha: shukrani na furaha ya  huruma na upendo wa Mungu kwa walimwengu. Kikundi hiki cha muziki kimepata kibali kutoka kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Albania, mahali anakozaliwa Mama Theresa wa Calcutta na kuungwa mkono na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kama alama ya shukrani kwa Mwenyezi Mungu kutokana na matendo yake makuu aliyolitendea Kanisa na walimwengu kwa njia ya maisha na utume wa Mama Theresa wa Calcutta.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.