2016-08-04 08:42:00

Siku ya Vijana Duniani 2019 Panama: Ushuhuda wa imani na Umissionari!


Baba Mtakatifu Francisko ametangaza kwamba, Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2019 itaadhimishwa nchini Panama, mwendelezo wa ari na ushuhuda wa kimissionari wa Mwenyeheri Oscar Arnulfo Romero, aliyeuwawa kikatili wakati akiadhimisha Ibada ya Misa Takatifu na sasa anaheshimiwa na Kanisa kuwa ni Mwenyeheri, mfano bora wa kuigwa katika kushuhudia imani hadi tone la damu.

Hivi ndivyo anavyosema, Kardinali Josè Luis Lacunza Maestrojuàn, Askofu wa Jimbo la David kwamba, mpango mkakati wa maisha na utume wa Kanisa nchini Panama unajikita katika upendeleo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii: kiroho na kimwili. Hiki ni kipaumbele cha pekee kinachotolewa na Baba Mtakatifu katika maisha na utume wake kwa wakati huu. Kwa kipindi cha miaka 40 iliyopita, Panama haikuwahi kupata kuwa na Kardinali hata mmoja, hadi mwaka 2015, Baba Mtakatifu Francisko alipomteua Askofu Maestrojuàn kuwa Kardinali, huku akimchagua kutoka katika Jimbo ambalo lilikuwa pembezoni mwa Nchi ya Panama.

Uchaguzi wa Baba Mtakatifu kuadhimisha Siku ya Vijana Duniani huko Panama, ni changamoto kwa Kanisa mahalia ili kujipanga vyema katika mchakato wa kuwapokea, kuwakirimia na kuadhimisha sherehe ya vijana kwa ari na moyo mkuu wa kimissionari kwa kuiga ujasiri wa Mwenyeheri Askofu mkuu Osca Romero. Kanisa linatarajia kwamba, kutakuwepo na umati mkubwa wa vijana kutoka Amerika ya Kusini watakaoshiriki katika maadhimisho haya kwa kuzingatia uchumi na uwezo wa vijana wenyewe.

Hata katika umaskini wao, vijana kutoka Amerika ya Kusini wataonesha jeuri ya imani kwa kushiriki kwa wingi katika sherehe hii ya imani. Umefika wakati wa kutoa kipaumbele kwa Kanisa changa kushuhudia imani, matumaini na mapendo yao kwa Kristo na Kanisa lake. Mwenyeheri Askofu mkuu Oscar Romero katika maisha na utume wake, alisimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu, akaonesha ushuhuda wa kuwa kweli ni Baba wa maskini na wale waliokuwa wanatengwa na kunyanyasika katika maisha.

Hii ni changamoto ya kusimama kidete pia kulinda na kudumisha haki msingi za binadamu, utu na heshima ya binadamu sanjari na kuendelea kuwa ni sauti ya kinabii kwa wale wasiokuwa na sauti! Ni wakati wa kuwajengea vijana Injili ya matumaini, imani na mapendo. Kanisa nchini Panama katika maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2019 linataka kushuhudia imani kwa Kristo na Kanisa lake kama sehemu ya mwendelezo wa Jubilei ya miaka 500 ya Uinjilishaji nchini Panama.

Kanisa nchini Panama lina nyuso za ujana, linaendelea kujizatiti katika ari na mwamko wa kimissionari na ni daraja la imani kwa nchi jirani. Panama ni chemchemi ya imani kwa familia ya Mungu Amerika ya Kusini, kumbe si haba kwamba, limekumbukwa kwa namna ya pekee na Baba Mtakatifu Francisko, mtu wa watu kwa ajili ya watu. Vijana wanaendelea kujisadaka katika mchakato wa Uinjilishaji mpya kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko ndani na nje ya Panama. Kanisa linaendelea kujipyaisha katika maisha na utume wake, kwa kusoma alama za nyakati!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.