2016-08-02 11:00:00

Ujana ni mali, msiuchezee kwani fainali uzeeni!


Maadhimisho ya Siku ya XXXI ya Vijana Duniani imekuwa ni changamoto kubwa kwa vijana sehemu mbali mbali za dunia kuwa ni mashuhuda, vyombo na mitume wa huruma ya Mungu kwa kujikita katika kanuni maadili, utu wema; umoja, haki, upendo na mshikamano, bila kusahau tunu msingi za maisha ya Kikristo! Kanisa linaendelea kuwekeza katika utume kwa vijana kwa kuhakikisha kwamba, vijana wanapendwa, wanathaminiwa na kuheshimiwa sanjari na kukuza majadiliano ya kina katika ukweli na uwazi na vijana ili kuwapatia dira na mwelekeo thabiti wa maisha yenye matumaini kwa leo na kesho iliyo bora zaidi.

Vijana wanapaswa kutambua kwamba, uhuru wa kweli unapatikana tu pale wanapomwambata Mwenyezi Mungu katika hija ya maisha yao. Yesu Kristo ndiye mlezi mkuu na mwaminifu kwa maisha ya vijana wa kizazi kipya, mwaliko na changamoto kwa vijana kukita maisha yao katika: Sala, Tafakari ya Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa sanjari na kumwilisha imani yao katika matendo kwa kushuhudia Fumbo la Msalaba, kielelezo kikuu cha huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu.

Ujana ni kipindi cha maswali na udadisi mkubwa, lakini wanakumbushwa kwamba, majibu ya kweli na haki kwa changamoto za ujana yametundikwa katika Fumbo la Msalaba. Vijana wanahitaji mashuhuda na walezi makini watakaoandamana nao katika hija ya maisha yao huku bondeni kwenye machozi huku wakishirikiana na vijana wenzao hadi kieleweke, ili kweli waweze kuwa ni mashuhuda na wajumbe wanaoaminika katika kutangaza na kushuhudia Injili ya amani, huruma na mapendo!

Jimbo Katoliki la Mbulu, Tanzania linaendelea kuwekeza katika malezi na makuzi ya vijana kwa kuimarisha Umoja wa Wanafunzi Wakatoliki, ili kuwawezesha vijana kutekeleza dhamana na majukumu yao kwa Kristo, Kanisa na Taifa katika ujumla wake. Padre Faustin Shauri mlezi na mwalimu wa Seminari Ndogo ya Sanu Jimbo Katoliki Mbulu wakati wa Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya TYCS, Wilayani Mbulu, Mkoani Manyara aliwataka vijana kujitambua, kujikubali sanjari na kuhakikisha kwamba, wanatekeleza mapenzi ya Mungu katika hija ya maisha.

Vijana watambue kwamba, wanapaswa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Mwenyezi Mungu kwani wao wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu! Wanao utu na heshima; mambo msingi ya kuzingatiwa katika maisha ya ujana. Padre Shauri anasema, Kanisa linapenda kuwatuma vijana ulimwenguni ili kuwa kweli ni vyombo, mashuhuda na wajumbe wa huruma ya Mungu kwa kujikita katika toba na wongofu wa ndani pamoja na utakatifu wa maisha, mambo yenye mvuto katika maisha ya ujana ambao kwa wengi wao sasa unaonekana kuchakaa kama kuti la mnazi!

Vijana wasimame kidetekulinda, kutetea na kudumisha kanuni maadili na utu wema kwani mbele yao kuna baraka na laana; kuna maisha, uzima na neema pamoja na kifo na mauti! Wawe na busara ya kuchagua njia inayowapeleka katika uzima wa milele kwa kusimamia na kushuhudia ukweli kama ilivyokuwa kwa Yohane Mbatizaji. Vijana wawe wachamungu, wema na watakatifu; mambo ambayo wanapaswa kuyapigania ili kushinda vishawishi vya ulimwengu mamboleo. Vijana wazingatie kanuni ya dhahabu kwa kutenda yale ambayo wangependa pia kutendewa na wengine! Vijana watangaze na kushuhudia upendo kwa Mungu na jirani, muhtasari wa mafundisho makuu ya Yesu. Vijana wawe ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu kwa vijana wenzao waliomezwa na malimwengu, ili waweze kuwavuta kimrudia Mungu, Kristo na Kanisa lake, kwa njia ya toba na wongofu wa ndani!

Mwishoni, Padre Faustin Shauri amewataka vijana kuwa mabalozi wema na watakatifu wa Kristo kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko kwa vijana wenzao. Vijana wawe na nidhamu katika kutumia muda wao wanapokuwa shuleni, ili kujipatia stadi za maisha, ujuzi na maarifa, tayari kushiriki katika ujenzi wa Kanisa na Jamii ya Tanzania katika ujumla wake! Maadhimisho ya TYCS Jimboni Mbulu yamefanyika wakati Kanisa linaadhimisha Siku ya XXXI ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2016, huko nchini Poland.

Na Sr. Editha Temu.

Jimbo Katoliki la Mbulu, Tanzania.








All the contents on this site are copyrighted ©.