2016-08-02 14:59:00

Padre Lombardi anawashukuru wadau wa tasnia ya habari!


Padre Federico Lombardi, SJ, aliyekuwa msemaji mkuu wa Vatican kwa muda wa miaka 10 na kung’atuka rasmi kutoka madarakani tarehe 31 Julai 2016, amewaandikia waandishi wa habari pamoja na wasaidizi wake wa karibu kuwashukuru kwa ushirikiano waliomwonesha wakati wote alipokuwa msemaji mkuu wa Vatican. Katika kipindi hiki cha miaka kumi, kwa pamoja wamekuwa bega kwa bega kufuatilia maisha na utume wa Papa Mstaafu Benedikto XVI na Baba Mtakatifu Francisko ambao walimwamini na kumpatia dhamana ya kuwa ni Msemaji mkuu wa Vatican.

Anawashukuru wale wote waliomsaidia, waliomtia shime katika utekelezaji wa dhamana na majukumu yake ya kila siku, wakati wa raha, uchungu na magumu ya maisha. Anamshukuru Mungu kwa kuweza kupokelewa na kusaidiwa katika maisha na utume wake bila kubaguliwa wala kutengwa. Hii ni dhamana kubwa ambayo ilikuwa inawajibisha sana anakiri Padre Lombardi na kusema kwamba, ameyafanya yote kama mtumishi asiye na faida na ametenda yale aliyopaswa kutenda na kwamba, ataendelea kusikiliza sauti ya wale ambao watapenda kwa jina la Kristo kumpatia dhamana nyingine tena.

Padre Lombardi anawashukuru na kuwapongeza wale wote wanaojisadaka katika uwanja wa mawasiliano ya jamii; kwa ajili ya huduma kwa jirani zao pamoja na dhamana inayoendana na wajibu huu. Mwishoni, Padre Lombardi anawatakia wadau wa mawasiliano ya jamii utume mwema na kwa namna ya pekee Bwana Greg Burke, Msemaji mkuu wa Vatican na Paloma Garcia Ovejero, Msemaji mkuu wa Msaidizi wa Vatican, katika utekelezaji wa dhamana na majukumu yao mapya mjini Vatican.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.