2016-07-28 13:58:00

Siku ya Vijana Duniani ni kielelezo cha amani, mshikamano na udugu!


Padre Federico Lombardi msemaji mkuu wa Vatican anabainishwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko amepewa mapokezi ya kukata na shoka wakati alipowasili nchini Poland, Jumatano tarehe 27 Julai 2016 tayari kushiriki katika maadhimisho ya Siku ya XXXI ya Vijana Duniani; Jubilei ya miaka 1050 ya Ukristo nchini Poland sanjari na Mwaka wa huruma ya Mungu. Baba Mtakatifu amezungumza na viongozi wa Serikali, Wanasiasa na Wanadiplomasia kwa kukazia umuhimu wa Injili ya uhai, shukrani kwa zawadi ya imani na kumbu kumbu endelevu ya historia ya familia ya Mungu nchini Poland.

Kilele cha Jubilei ya miaka 1050 Ukristo nchini Poland ni tukio ambalo limekuwa na mvuto mkubwa kwa familia ya Mungu ndani na nje ya Poland. Baba Mtakatifu amekutana na kuzungumza na Baraza la Maaskofu Katoliki Poland na kusaidia kujibu dukuduku za maisha na utume wa Kanisa katika ulimwengu mamboleo: kiroho, kimwili na kitamaduni. Kwa namna ya pekee anasema Padre Lombardi, Baba Mtakatifu amekazia umuhimu wa kujenga na kudumisha umoja, upendo na mshikamano wa kitaifa pamoja na huduma makini kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii, kielelezo cha uwepo endelevu wa Kristo kati ya watu wake.

Waamini wanahamasishwa na Baba Mtakatifu kukita maisha yao katika Heri za Mlimani, muhtasari wa Mafundisho makuu ya Yesu kwa wafuasi wake pamoja na kumwilisha matendo ya huruma katika uhalisia wa maisha ya watu, kwani hiki ndicho kipimo atakachotumia Yesu atakapokuja kuwahukumu wazima na wafu! Kumbe, dhana ya huruma ya Mungu ni kiini cha mafundisho ya Baba Mtakatifu Francisko, mwendelezo wadhana ya huruma ya Mungu kama ilivyoasisiwa na Mtakatifu Yohane Paulo II na Sr. Faustina.

Ukarimu na huduma kwa wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta hifadhi ya maisha yao. Poland inapata wahamiaji na wakimbizi kutoka Ukraine na Russia; kumbe hapa suala la wakimbizi kutoka Afrika au changamoto ya kidini si tatizo kubwa kwani wengi wa wakimbizi na wahamiaji hawa ni wananchi kutoka Bara la Ulaya na wengi wao ni Wakristo wa Makanisa mbali mbali. Hapa ndiyo maana Baba Mtakatifu Francisko anakazia umuhimu wa Kanisa kujenga na kudumisha utamaduni wa ukarimu na Injili ya huruma na mapendo.

Wahamiaji na wakimbizi hawa ni wale wanaotaka kusalimisha maisha yao kutokana na vita, hali ngumu ya maisha pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi. Hata katika maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kuna vijana kutoka dini, tamaduni na lugha mbali mbali wanaotaka kusikiliza neno la faraja na matumaini kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko. Hapa Kanisa linajitahidi kujenga madaraja ya watu kukutana ili kufahamiana, kuelewana na hatimaye kudumisha haki, amani na maridhiano kati ya watu. Wote hawa wanafumbatwa katika dhana ya huruma ya Mungu isiyokuwa na ubaguzi kwa mtu awaye yote!

Padre Lombardi anakaza kusema, maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani ni wakati wa imani, matumaini  na mapendo; ni muda wa kushuhudia ujasiri na amani, ujumbe ambao vijana wanataka kuusambaza kwa walimwengu ambao kwa sasa wamegubikwa na wasi wasi pamoja na hofu ya mashambulizi na vitendo vya kigaidi. Walimwengu wana kiu ya haki, amani na maridhiano na wala si vita wala kinzani na mipasuko ya kijamii.Maadhimisho ya Siku ya Vijana ni Ujumbe wa amani, upendo na mshikamano kati ya vijana wa kizazi kipya. Huruma ya Mungu ni kiini cha maadhimisho haya dhidi ya kuta za utengano, chuki na uhasama. Hiki ni kipindi cha kujikita na kushuhudia amani dhidi ya kinzani na chuki zisizokuwa na mashiko wala mvuto kwa ustawi na maendeleo ya wengi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.