2016-07-27 14:30:00

Wataona macho kwa mirathi!


Mara nyingi wakati wa msiba kunazuka sokomoko na sintofahamu ndani familia moja linapokuja suala la kugawana mali za marehemu. Wanafamilia wanagombana na mwisho kufarakana. Namna yetu ya kugawana mali na mirathi, hata kama kwa kufuata utaratibu wa kitamaduni, au kifamilia, au kisheria za nchi mara zote haujali mahitaji ya wanaogawana. Kwa hiyo kama mali yangegawiwa kwa haki, lakini watafamilia wanabaki kununiana kwa maisha yote. Hii ndiyo hali halisi ya mtu na mali. Wakati wa Yesu mambo hayakuwa tofauti. Katika kesi za kugawana mali ya mirathi, Marabi ndiyo walikuwa wasuluhishaji na walikuwa wanapata komisheni inayoeleweka kama ilivyo kwa mahakimu na ma-advocate wa siku za leo. Kwa vile Yesu ni Rabi (mwalimu) watu walimwendea ili wasaidiwe kusuluhisha ugomvi wao wa mirathi.

Leo, Yesu analetewa kesi ya mirathi toka kwa kaka mdogo, kwani kadiri ya sheria za nchi na mila na desturi za Wayahudi kuhusu mirathi, kaka mkubwa alisubiri kupata theluthi mbili na kaka mdogo aligawiwa theluthi moja ya mirathi. Kwa hiyo,“Mtu mmoja katika mkutano akamjia Yes una kkamwambia:“Mwalimu mwambie ndugu yangu anigawie urithi wetu.” Huyu kijana mdogo anamtaka Yesu amwambia kaka yake afuate sheria za mirathi, amgawie katheluthi kake anakostahili. Hapa ningekuwa mimi ndiye Rabi, ningesema tu kirahisi kwamba sheria ya mirathi ichukue mkondo wake na kijana apate mshiko wake na wala wasitafutane ubaya na kutibuana chongo bure. Huu ni utatuzi wa hekima sana kadiri ya haki na sheria zilizopangwa na binadamu, kama tulivyozoea kusikia “mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni.”

Kumbe, kasoro ya mtindo huu wa kugawana mirathi hautatui tatizo la mpasuko katika familia. Yesu anataka kuingia kwenye kiini cha mpasuko na mfarakano ndani ya familia au ndani ya jumuia katika masuala ya mirathi na mali kwa ujumla. Yesu anajiweka kando bila kuingilia kati shauri hilo, anajibu: “Mtu wewe,” Huyu mtu hatajwi jina, kwa sababu hapa Yesu anamkabili kila binadamu. Anamwambia “ni nani aliyeniweka mimi kuwa mwamuzi au mgawanyi juu yenu?” Ni mahali pekee katika biblia, unapoona neno hili “mgawanyi.” Halafu anauliza “Ni nani” akimaanisha mtu fulani. Katika kesi hii inamhusu Mungu. Anataka kusema “Mungu ndiye aliniweka niwe mwamuzi na mgawanyi wa mirathi yenu kwa kutumia vigezo vyenu, ambavyo vinasababisha mafarakano kati yenu.”

Kumbe, mali ya duniani hii ni urithi aliotupatia Mungu hautakiwi ugawanywe kadiri ya vigezo vya kibinadamu bali kadiri ya mawazo na mpango wa Mwenye Mungu. Kugawana mali kwa vigezo vya kibinadamu hutusababishia: vita, chuka, mafarakano na mipasuko ya kijamii. Mali hizo nyingi tulizotupata toka kwa Mungu ni kama vile akili, maweza yetu, vipaji vyetu mbalimbali nk. Kwa hiyo sisi sote tumetajirishwa bure na lakini pia tupo fukara yaani tumepokea na tunatoa. Mungu ametufanya kuwa tajiri ili kutoa kwa wengine, ili kujenga misingi ya haki, amani, upendo na umoja. Kwa maneno machache, utajiri wa binadamu unapaswa kuwa ni chombo cha huruma ya Mungu kwa maskini wa kiroho na kimwili!

Kisha Yesu anatahadharisha: “Angalieni, jilindeni (kuwa tayari daima) na choyo.” Neno hili choyo ni tafsiri potovu, kwani neno la Kigiriki pleoneksia, maana yake ni ugonjwa wa kujilundikia mali na kudhani kuwa duniani ni mahali petu! Pleoneksia ni msukumo unaokufanya upoteze kichwa na kuchanganyikiwa mbele ya mali. Watu wanalinganisha kufaulu kwa maisha kwa kuwa na mali na utajiri mkubwa na kusahau kwamba, pengine hata hao wenye mali hawapati lepe la usingizi hata kidogo. Kumbe, Pleoneksia hiyo inatokana na woga wa kifo unaotuvutia kwenye kuthamini mali badala ya kuthamini maisha.

Kisha Yesu anatoa mfano wa mkulima aliyefanikiwa kuwa na tajiri sana: “Shamba la mtu mmoja tajiri lilikuwa limezaa sana” Kwa vyovyote mkulima huyu alikuwa anafanya kazi usiku na mchana, hadi kufanikiwa kuchuma mali mengi. Mali ni alama ya kubarikiwa na Mungu kama ilivyoelezwa katika Kumbukumbu la Torati 28. Kwa hiyo mkulima huyu alikuwa tajiri wa haki, wala hakuwa mbaya wala fisadi na mkwepa kodi bali alikuwa analipa kodi na pengine alikuwa mcha Mungu mzuri tu. Mbele ya macho ya ulimwengu, mtu huyu amefaulu, ameukata, ameulamba, Mwenyezi Mungu ampe nini tena? Gunia la chawa ajikun? Kwa sababu anayo mali. Kumbe, katika utajiri huo kukajitokeza tatizo.

Mtu huyo“akaanza kuwaza moyoni mwake, akisema, nifanyeje maana sina pa kuyaweka akiba mavuno yangu?” Tatizo la mtu huyu siyo kuwa na mali, bali atafanya nini na mali hiyo. Kumbe mtu huyu hana furaha kutokana na mali yake. Analalamika na kulala hoi kwa mawazo kama wanavyolalamika fukara wengine tunaowasikia wakisema:“Nitafanya nini, sijui nitakula nini, sina nguo, sina maji, sina fedha nk. Mtu anayejilundikia mali na kujiuliza: nitafanya nini na mali yangu, hapo ujue dhamiri inamwuma kwa sababu mali hiyo ni ya fukara. Utatuzi wa haraka katika mazingira kama hayo ni kufungua milango yote ya ghala na kuwagawia fukara, kitendo hicho kingemtengenezea marafiki wengi sana. Kinyume chake, mtu huyu anaamua kujenga ghala kubwa zaidi na kuziba kila mwanya isitoke hata chembe ya chakula wala mali. Kisha anakumbuka kuwa anahitaji kupumzika na kutulia anajisemea dhamirini mwake: “Tulia moyo wangu, ule unywe.” Ati ponda mali kufa kwaja! Programu ya maisha yake sasa ni kutulia kula na kunywa. Kumbe, maisha yake yote yalikuwa ni kazi tu ya kuchuma na kujilimbikizia mali.

Mtu huyu  ni mpweke sana na yuko yeye na mali basi. Unashangaa hata huioni familia yake ikitajwa, yaani mke na watoto, wala wafanya kazi wake, bali yuko yeye peke yake amezamiria kuchuma mali tu hata hakujali familia au jumuiya yake. Aliishi kati ya watu lakini hakuwaona kwani aligubikwa na upweke hasi, dalili za kifo! Kwake hakuna watu, hakuna Mungu bali ni mali tu. Ukipata muda wa kusoma Injili na kuchunguza lugha ya mtu huyu, utaona amezungumza maneno hamsini na tisa. Kati ya maneno hayo yote, maneno kumi na nne yamejaa mimi, yangu. Hayo ndiyo mapato ya Pleoneksia., tatizo la mtu kujitafuta na kujiangalia mwenyewe!

Sasa tuione nafsi ya tatu, ambayo ni Mungu mwenyewe jinsi anavyomwangalia mtu huyu na mali yake. Mungu anamwangalia mtu huyu na kutikisa kichwa kwa dharau sana: “Mpumbavu wewe.” Neno la kigiriki ni “aphron” maana yake siyo tu mpumbavu, mjinga, mbumbumbu, bali ni bwege, mwenda wazimu, chihimwisi na mtu wa kuja! Kwa vyovyote hatua hii ya aphron aliyofikia mgonjwa huyu, Mungu asingeweza kumlaani wala kumchukua kwani ingekuwa ni kumwonea bure kwa vile mgonjwa wa pleoneksia. Hata kama ni kufa huwezi kusema eti “Bwana ametoa, Bwana ametwaa, Jina la Bwana litukuzwe” kwani hapa Mungu hausiki kabisa. Kwa vyovyote kutokana mahangaiko ya kazi, bila kupumzika, halafu wasiwasi juu ya kuongeza mali na kuyatunza, ni dhahiri kabisa mtu huyu alikufa au kwa shinikizo la damu, au pumu, au moyo kusimama ghafla kama inavyowatokea wengi. Alijisahau katika mali hakujua kama mali hiyohiyo inaweza kumtumbua siku moja.

Mtu huyu ni ”bwege” tena mtozeni” kwa sababu alidhani kwamba atamiliki mali hiyo kwa milele, bila kufikiria kwamba muda wa kumiliki mali hiyo una kikomo chake. Ukifika mpakani mwa nchi wanapocheki mizigo, mali haramu hairuhusiwi kupitishwa. Ugonjwa wa preloneksia unakuondolea kichwani mawazo kwamba, maisha haya hayana mwisho, bila kutambua kwamba mali yapo kwa ajili ya kujaza sanduku la upendo, ambapo mpakani linapita bila matatizo. Mtu huyu alimbadilisha Mungu na miungu ya mali yake akaishia kuwa bwege.

Yesu anasema “Fanyeni mifuko isiyoweza kuharibika kwani Sanda haina mfuko hata siku moja.” Yaani kufanya matendo ya huruma, na ya upendo. Kinachojalisha siyo kile tulicho nacho bali kile tulichotoa. Kwa hiyo busara anayotupata Yesu siyo kumiliki bali kutoa. Hazina ya ulimwengu huu haitupeleki mbali isipokuwa kwenye kuwa mabwege na mapato yake kufarakanisha jamaa na jumuiya za watu!

Na Padre Alcuin Nyirenda, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.