2016-07-26 08:56:00

USCCB : Juhudi mpya za kukuza amani na umoja Marekani


(WASHINGTON-) Katika mwanga wa matukio ya hivi karibuni ya vurugu na mvutano wa rangi katika jamii ya Marekani, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki  Marekani(USCCB) ametoa mwaliko kwa majimbo yote nchini Marekani, kuungana katika Siku ya Maombi ya Amani katika Jumuiya zote za Kanisa.  Na pia kumeteuliwa Tume  maalum ya kazi, ili kwamba, baada ya Siku ya Maombi,kuwe mwendelezo wa utendaji mapana zaidi, kwa ajili ya kukuza amani na uponyaji kwa roho zilizoumizwa na matatizo makubwa yenye kuigawa  jamii ya marekani.

Tume hiyo iliyoundwa ni  kwa ajili ya kupata majibu  ya haraka  katika kukabili mashabulizi ya kutumia sialha za moto,kama bunduki kwa misingi ya ubaguzi wa rangi, kama ilivyofanyika huko Baton Rouge, Minneapolis na Dallas.   Askofu Mkuu Joseph E. Kurtz ya Louisville, Kentucky, katika maoni yake ya haraka  haraka juu ya jambo hili, alitaja haja kwa Kanisa Katoliki kutazama njia itakayoliwezesha Kanisa Katoliki kuwaunganisha watu na kutoa msaada wa kiroho katika siku hizi za mateso kwa jamii ya Marekani.

Alisistiza kutazama mbinu za ziada katika njia ya malezi wazi kwa waamini na watu wote kwa ujumla, ambamo wataweza kutengeneza nafasi ya mazungumzo ya wenyewe kwa wenyewe juu ya masuala ya mahusiano ya kijamii, ujenzi wa haki, afya ya akili, fursa za kiuchumi, na kutazama kwa jinsi gani inawezekana kusitisha kuenea kwa vurugu za kutumia bunduki. Askofu Mkuu Kurtz alisema, ni kuwa na Siku ya Maombi na baada ya hapo majadiliano yaendelezwe kwa msaada wa kikosi maalum cha kazi  katika upande huo, kama hatua ya uponyaji kwa wale wanaoendelea kukumbatia mateso  na chuki, waweze kuondokana na hali hiyo,  kupitia umoja wenye kuhamasishwa na hatua madhubuti za upendo wa Kristo. Maaskofu wanatumaini kufanikisha amani na kujenga madaraja ya mawasiliano na utoaji wa misaada kwa  pande zote za  jamii ya Wamarekani.

Siku ya Maombi ya Amani katika Jumuiya zote za Marekani itafanyika tarehe 9 Septemba ambamo Mama Kanisa huadhimisha sikukuu ya Mtakatifu Petro Claver,  na itatumika kama kitovu cha  nguvu kazi. Kikosi hiki cha kazi  kinalenga kuwasaidia maaskofu kujihusisha kwa ukaribu zaidi  na matatizo na changamoto za kijamii moja kwa moja, kupitia njia mbalimbali kama : kukusanya na kusambaza msaada,  kuunga mkono "mbinu bora"; kusikiliza kwa makini  matatizo ya  jumuiya zenye wasiwasi, msaada katika utekelezaji wa  sheria; na ujenzi wa  uhusiano imara,  ili kusaidia kuzuia na kusuluhisha migogoro. Kikosi cha kazi baada ya kuhitimisha kazi yake kitatoa ripoti  juu ya shughuli zake na mapendekezo kwa ajili ya utendaji wa  baadaye, ripoti itakayojadiliwa katika Mkutano Mkuu wa USCCB  mwezi  Novemba.

Askofu Mkuu Wilton D. Gregory wa Atlanta, rais wa zamani USCCB, atakuwa mwenyekiti wa kikundi kazi. Akiipokea utume huo mpya Askofu Mkuu Gregory amesema kwake ni jambo la  fahari kushughulika na juhudi hizi mpya kwa ajili ya kutoa msaada kwa Maaskofu wenzake kama mmoja mmoja na kama kikundi, kuongozana pamoja na mateso ya jamii katika njia inayoelekea kujenga  amani na maridhiano. Wao ni mwili mmoja katika Kristo, hivyo wanapaswa kutembea na wote wake kwa waume katika kujenga dhamira mpya,  kukuza uponyaji dhidi ya mateso si mahali pengine, au mtu mwingine ila kati yao wenyewena  katika majimbo yao wenyewe.

Wajumbe wengine katika Tume hii ya kazi ni Askofu Mkuu Thomas G. Wenski ya Miami, Mwenyekiti wa Kamati ya USCCB juu ya Maendeleo ya ndani ya Jamii; Askofu Shelton J. Fabre ya Houma-Thibodaux, Louisiana, mwenyekiti wa USCCB Kamati Ndogo kwa masuala yanayohusiana na Wamarekani wenye asili ya Afrika; Askofu John H. Ricard, SSJ, Mstaafu Askofu wa Pensacola-Tallahassee, Florida, mwenyekiti wa zamani wa USCCB Kamati Ndogo ya Kanisa la Afrika, na Mjumbe  wa USCCB katika Kamati Ndogo kwa masuala ya Wamarekani wenye asili ya Afrika, na mjumbe katika bodi ya Kitaifa Taifa  ya Kongress ya Wakatoliki wenye asili ya Afrika ; na Askofu Jaime Soto wa Jimbo la California, mwenyekiti wa USCCB Kamati Ndogo ya Kampeni Katoliki kwa Maendeleo ya Binadamu (CCHD).

Kikosi cha Kazi,  pia kina wajumbe mbalimbali washauri, ikiwa ni pamoja na Makamu wa Rais wa USCCB  Kardinali Daniel N. DiNardo wa Galveston-Houston.  








All the contents on this site are copyrighted ©.