2016-07-26 14:09:00

Papa asikitishwa kwa mauaji ya P. Hamel huko Ufaransa!


Kwa mara nyingine tena Ufaransa imetikiswa na mauaji ya kigaidi dhidi ya watu watatu, akiwepo Padre Jacques Hamel, 84 na watu wengine wawili waliohusika na mauaji haya ya kinyama. Watu wengine walijeruhiwa vibaya na mmoja wao, inasemekana kwamba, hali yake ni mbaya! Mauaji haya ya kigaidi yametokea, Jumanne, tarehe 26 Julai 2016 huko nchini Ufaransa, kwenye Kanisa la Saint-Etienne du Rouvray, Jimbo Kuu la Rouen.

Padre Lombardi, Msemaji mkuu wa Vatican anasema, Vatican imepokea habari za mauaji haya ya kigaidi kwa masikitiko makubwa kwani umekuwa ni mfululizo wa mauaji ya watu wasiokuwa na hatia. Wasi wasi na hofu vinaendelea kutanda. Baba Mtakatifu amejulishwa tukio hili na amesikitishwa sana na anapenda kwa mara nyingine tena kuchukua fursa hii kulaani kwa ngvvu zote vitendo vyote ya kigaidi vinavyoendelea kusababishya maafa, mateso na nyanyaso dhidi ya utu na heshima ya binadamu.

Baba Mtakatifu anasali kwa ajili ya wale wote walioguswa na msiba huu mzito. Inasikitisha sana kwani mauaji haya yamefanyika ndani ya Kanisa, mahali patakatifu ambamo upendo wa Mungu unatangazwa na kushuhudiwa! Ameuwawa Padre na waamini wake kujeruhiwa vibaya. Baba Mtakatifu anasema, yuko karibu na familia ya Mungu nchini Ufaransa na kwa namna ya pekee kabisa, Jimbo kuu la Rouen pamoja na Jumuiya ya Kikoptik.

Kwa upande wake, Askofu mkuu Dominique Lebrun wa Jimbo kuu la Rouen ambaye kwa sasa yuko nchini Poland kuhudhuria maadhimisho ya Siku ya XXXI ya Vijana Duniani, ameamua kurejea Jimboni mwake, ili kuungana na familia ya Marehemu Padre Jacques Hamel pamoja na Jumuiya nzima ambayo kwa sasa imepigwa na bumbuwazi kubwa! Kanisa halina silaha dhidi ya magaidi, bali litaendelea kusali, kujenga na kudumisha umoja. Anawataka vijana kutokubali kuingizwa katika mnyororo wa vitendo vya kigaidi vinavyodhalilisha maisha, utu na heshima ya binadamu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.