2016-07-25 14:16:00

Kardinali Tauran asema :ni tu utamaduni wa kukutana unaoweza kushinda chuki na ugaidi


Kushinda moyo wa chuki na ugaidi , hakuna jawabu zaidi ya kupenda utamaduni wa kukutana na majadiliano.  Ni maoni yaliyotolewa na Kardinali Jean Luis Tauran , Rais wa Baraza la Kipapa, kwa ajili ya majadiliano kati ya dini wakati akijibu maswali ya Mare Duhamel, Jumamosi iliyopita, juu ya mashambulio ya kigaidi,  yanayosikika kila kukicha hapa na pale na hivyo kuleta hofu kubwa kwa usalama wa watu. 

Kardinali naye aliuliza kuna nini kwa binadamu wa leo na  i wapi thamani ya maisha ya binadamu? Je binadamu ameumbwa kwa ajili ya kifo? Alisema ghasia hizi za fujo na mauaji zinazua maswali mengi kwa watu wenye mapenzi mema, kutaka kujua iwapo watu wa leo wanathamani maisha. Kardinali Tauran alieleza na kuonyesha kujali kwa jinsi leo hii, wakati wote umekuwa ni  wakati wa hatari za kifo. Mazingira ya kufikira yamebadilishwa na kuwa tofauti na wakati wa wahenga ambao waliishi na msemo kwanza maisha na baadaye kifo. Wakati huu msema huo hauna tena maana muda wote umekuwa ni wakati wa kifo, hakuna tena  kuaminiana kiusalama, binadamu amekuwa kweli adui wa binadamu mwingine. Ukitoka nyumbani kwako hakuna tena uhakika wa kurudi salama nyumbani.  Hii ndiyo hali halisi wanayoiishi watu kwa wakati huu.

Kardinali anasema ili kuondokana na hali hiyo ya wasiwasi , unakuwa ni wajibu kwa watu wote na hasa kwa familia kuelimishana na hasa ndani ya familia kuelimisha maana ya maisha binadamu na heshima yake.  Na pia ni muhimu kwa watu kusoma historia kwa kina, si kupaparuka tu na utendaji, lakini watu lazima kuwa na ufahamu kwamba, tunapaswa kuzingatia kwamba,  sisi ni sehemu ya mwendelezo wa historia ya jumuiya yetu na binadamu kwa ujumla. Hivyo haifai kurudia matukio yaliyokwisha onekana kuwa nje ya misingi ya ubinadamu.

Kardinali Taurani aliendelea kuzungumzia umuhimu wa kushirikiana kutoa ufafanua kifilosofia, umuhimu wa kukutana na kuzungumza pamoja, kama wana wa Mungu mmoja kwa kuwa ni Mungu mwenyewe ndiye mwenye kuingoza historia ya binadamu na mwenye kujua hatma ya kila binadamu.

Ndiyo maana inafaa sasa , wakati huu kufanya kila linalowezekana kukutana na kuzungumza kwa pamoja kama jibu la kusitisha ghasia na mauaji haya yanayoendelezwa kila siku. Mtu anatakiwa kuona sababu za  kubadilisha mtindo wake wa maisha, na hasa kupata wogofu wa moyo. Kardinali Tauran ameeleza na kumshukuru Mungu kwa imani aliyonayo kwamba,  kifo si hatima ya maisha ya mtu.  

 








All the contents on this site are copyrighted ©.