2016-07-23 08:15:00

Papa Francisko hujaji wa huruma ya Mungu nchini Poland


Kardinali Pietro Parolin Katibu mkuu wa Vatican katika mahojiano maalum na kituo cha Televisheni cha Vatican, CTV anasema, hija ya 15 ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Poland kama sehemu ya maadhimisho ya Siku ya XXXI ya Vijana Duniani inaongozwa na kauli mbiu “Heri wenye rehema maana hao watapata rehema”. Hii ni hija inayofumbata maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, mahali alipozaliwa Mtakatifu Yohane Paulo II muasisi wa Siku ya Vijana Duniani na mtume hodari wa huruma ya Mungu.

Baba Mtakatifu Francisko anataka kuendeleza nyayo za Yohane Paulo II kwa kukoleza maisha na utume wa Kanisa miongoni mwa vijana wa kizazi kipya kwa kukazia umuhimu wa kumwilisha tunu msingi za maisha ya Kiinjili katika maisha ya vijana; Sakramenti za Kanisa hasa Ekaristi Takatifu na Upatanisho pamoja na kuwasaidia vijana kuyafahamu Mafundisho ya Kanisa dira na mwongozo thabiti kwa waamini katika safari ya utakatifu wa maisha. Dhana ya huruma ya Mungu ni urithi mkubwa ambao Mtakatifu Yohane Paulo II ameliachia Kanisa katika kipindi hiki cha mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo!

Kardinali Parolin anakumbusha kwamba, Waraka wa kitume “Huruma ya Mungu” “Dives in Misericordia”;  alipomtangaza Sr. Faustina Kowalska kuwa Mtakatifu sanjari na kuanzisha Jumapili ya huruma ya Mungu ni mambo ambayo yanaendelezwa na Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wa Kanisa, lakini kwa namna ya pekee wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Huu ni mwaliko kwa vijana kujiaminisha kwenye huruma ya Mungu kama alivyokuwa anasali Mtakatifu Faustina. Lengo ni kuwawezesha vijana kujenga utamaduni wa kukutana na Mwenyezi Mungu kwa njia ya: Sala, Tafakatifu, Sakramenti za Kanisa na matendo ya huruma.

Baba Mtakatifu Francisko akiwa nchini Poland atapata nafasi ya kutembelea na kusali kwenye Madhabahu ya huruma ya Mungu; ataungamisha vijana, ili kuwashirikisha huruma ya Mungu inayobubujika kutoka katika Sakramenti ya Upatanisho pamoja na kusali katika maeneo ambamo aliishi Mtakatifu Faustina na kubahatika kujipatia tasaufi ya Yesu mwenye huruma na hatimaye, Baba Mtakatifu pamoja na mahujaji wengine wote wataweza kupitia kwenye Lango la huruma ya Mungu.

Hija ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Poland inajikita katika mambo makuu mawili: kwanza ni maadhimisho ya Siku ya XXXI ya Vijana Duniani. Ujumbe wa Baba Mtakatifu kwa vijana wote ni kujenga moyo wa matumaini kama sehemu ya mchakato wa kupambana na changamoto zinazoendelea kujitiokeza na kwa namna ya pekee Barani Ulaya. Hapa, Jumuiya ya Ulaya inahamasishwa kugundua tena urithi na utajiri wake wa tunu msingi za maisha ya Kikristo, kwa kukazia utu na heshima ya binadamu bila kutelekeza haki zake msingi.

Baba Mtakatifu anataka kuwahamasisha vijana kutangaza, kushuhudia na kumwilisha Injili katika maisha na vipaumbele vyao sanjari na kukabiliana na matatizo, changamoto na fursa mbali mbali kwa mwanga wa Injili. Huu ni mwaliko pia wa kupambana na umaskini, ukosefu wa fursa za ajira, lakini zaidi ni mapambano dhidi ya umaskini wa kimaadili ambao ni hatari kubwa katika ulimwengu mamboleo.

Pili, Baba Mtakatifu Francisko akiwa mjini Czestochowa atashirikiana na familia ya Mungu nchini Poland kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa kuadhimisha Jubilei ya miaka 1050 ya Ukristo. Kutokana na sababu za kisiasa, familia ya Mungu nchini Poland ilipokuwa inaadhimisha Jubilei ya miaka 1000 ya Ukristo, Mwenyeheri Paulo VI hakuruhusiwa kwenda kuhudhuria maadhimisho haya.

Lakini miaka 50 baadaye, Baba Mtakatifu Francisko anaungana nao ili kumshukuru Mungu kwa zawadi ya imani, uhuru pamoja na uhuru wa kuabudu unaoiwezesha familia ya Mungu nchini Poland kushuhudia imani yake, huku ikiwa imeungana na viongozi wake wa Kanisa. Nchini Poland kuna wazazi na walezi wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Injili ya familia; kuna vijana waliobobea katika maisha na utume wa Kanisa.

Kimsingi nchini Poland, Kanisa linaendelea kusonga mbele kwa ari na mwamko mkubwa katika maisha ya Kikristo, utume na ari ya kimissionari. Kuna changamoto nyingi zinazotokana na utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Ukanimungu ni kati ya changamoto kubwa zinazowakabili wananchi wa Poland kwa wakati huu kwani kuna watu wanafikiri na kutenda kana kwamba, hakuna Mungu. Hapa kuna haja kwa Kanisa la Poland anasema Kardinali Parolin kuwa na kipaji cha ugunduzi na uwazi ili kukabiliana na changamoto hizi katika maisha!

Baba Mtakatifu anapata nafasi ya kutembelea kwenye kambi za mateso na mauaji ya kinyama huko Auschwitz na Birkenau. Ataadhimisha kumbu kumbu ya miaka 75 tangu Mtakatifu Marximillian Maria Koble alipouwawa kikatili bila kusahau mauaji ya kimbari dhidi ya Wayahudi. Hapa Baba Mtakatifu anaomba ukimya, ili kupata nafasi ya kutafakari ukatili dhidi ya utu na heshima ya binadamu. Baba Mtakatifu anataka kuikumbusha Jumuiya ya Kimataifa kwamba, hata leo hii bado kuna vita, nyanyaso, dhuluma na kufuru dhidi ya utu, heshima na haki msingi za binadamu.

Kardinali Parolin anasema, Jumuiya ya Kimataifa inaendelea kushuhudia vitendo vya kigaidi, kinzani na mipasuko ya kijamii; mambo ambayo wakati mwingine yanasababishwa na masilahi ya kisiasa na kiuchumi pamoja na kuendeleza biashara haramu ya silaha. Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kulihamasisha Kanisa kuwa karibu na watu wanaoteseka: kiroho na kimwili, lakini zaidi kwa watoto wadogo ambao wanapaswa kuonjeshwa huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao.

Akiwa nchini Poland, Baba Mtakatifu atatembelea Hospitali ya Watoto ili kuwaonjesha huruma na upendo wa Mungu, mwaliko kwa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuwa ni Wasamaria mwema kwa kutambua na kuguswa na shida pamoja na mahangaiko ya jirani zao.  Haya ndiyo mambo makuu ambayo Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuyakazia wakati wa hija yake ya kitume nchini Poland kuanzia tarehe 27 – 31 Julai 2016.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.