2016-07-22 15:25:00

Siku kuu ya Mt. Maria Magdalena: Siku ya shukrani kwa wanawake!


Askofu mkuu Arthur Roche, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Ibada na Nidhamu ya Sakramenti za Kanisa anasema, Siku kuu ya Mtakatifu Maria Magdalena, mtume wa mitume inayoonesha jinsi alivyoguswa na huruma ya Mungu inayoponya na kuokoa kutoka katika lindi la dhambi hadi kuwa ni shuhuda na mtume wa huruma ya Mungu kwa mwanadamu.

Tarehe 22 Julai 2016 kwa mara ya kwanza Kanisa linasali na kuwaombea wanawake wote walioonesha ujasiri wa pekee katika kumwamini, kumpenda na kutangaza Kristo Yesu kwa njia ya maisha yao kwa watu wa nyakati mbali mbali duniani. Kweli ni vyema na haki kumshukuru Mwenyezi Mungu kutokana na utukufu wake ulioshuhudiwa na Kristo Yesu na kutangazwa na Mtakatifu Maria Magdalena. Akabahatika kuwa mtume kwa mitume wa Yesu waliokimbia mbio kwenda kushuhudia kaburi wazi, Kristo Yesu akiwa amefufuka kwa wafu! Maria Magdalena alibahatika kumwona Yesu “Live” yule aliyekuwa amempenda wakati wa uhai wake, akashuhudia akiteswa, kufa na kuzikwa. Akabahatika kumwabudu akiwa amefufuka kwa wafu kama anavyosimulia Mwinjili Yohane. Maria Magdalena akawa ni shuhuda wa Injili hai, yaani Kristo Yesu, Bustani iliyokuwa chanzo cha kifo wakati wa Eva na Adamu, sasa inakuwa ni chemchemi ya maisha na Injili ya furaha!

Ndani ya Kanisa kuna wanawake mashuhuda waliosikia majina yao yakiitwa na Kristo Yesu katika maisha na utume wa Kanisa, leo hii wanapumzika kwenye usingizi wa amani huko mbinguni. Huu ni mwaliko kutoka kwa Shirikisho la Wanawake Wakatoliki Duniani pamoja na Jukwaa la Wanawake Wakatoliki Duniani kuwaenzi wanawake hawa kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko katika maisha yao kwa njia ya huduma makini kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Wanawake wamekuwa mstari wa mbele katika kukuza na kudumisha maisha na utume wa Kanisa katika ngazi mbali mbali za maisha. Hii ni siku ambayo Mama Kanisa anapenda kuwashukuru wanawake wote kwa moyo na upendo wao wa kimama katika maisha na utume wa Kanisa. Wanawake wanaalikwa kuendelea kuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu kwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Wanawake waendelee kuwa ni mfano na kikolezo cha utakatifu wa maisha katika sehemu mbali mbali za dunia na kwamba, utakatifu ni jambo linalowezekana, kila ajitahidi kutekeleza dhamana na wajibu wake baranara katika maisha  na utume wa Kanisa na katika majukumu ya kifamilia na kijamii.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.