2016-07-15 14:38:00

Boko haramu ni changamoto kubwa kwa amani na usalama Nigeria


Nigeria ni kati ya nchi za Afrika ambazo zimebahatika kuwa na utajiri mkubwa wa maliasili na rasilimali watu. Inakadiriwa kwamba, idadi ya wananchi wa Nigeria kwa sasa ni zaidi ya millioni 170 na kati yao millioni 20 ni waamini wa Kanisa Katoliki. Lakini changamoto kubwa kwa wakati huu nchini Nigeria ni haki, amani, ustawi na maendeleo ya wengi yanayokwamishwa na mashambulizi ya kigaidi yanayofanywa mara kwa mara na Kikundi cha Kigaidi cha Boko Haram ambacho kwa sasa kimekuwa ni tishio kubwa la usalama na mafungamano ya kijamii huko Afrika Magharibi.

Katika kipindi cha miaka 7, Boko Haram imesababisha vifo vya watu zaidi 20, 000 na watu wengine millioni 2. 6 hawana makazi ya kudumu, kiasi kwamba wamegeuka kuwa ni wakimbizi na wahamiaji hata katika nchi yao wenyewe! Yote haya ni matokeo ya rushwa na ufisadi wa mali ya umma; Uchu wa mali na madaraka unaojikita katika ubinafsi usioguswa na mateso ya wengi. Askofu mkuu Ignatius Kaigama, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria katika mahojiano maalum na Shirika la Kipapa kwa ajili ya Makanisa hitaji anasema, hizi ni kati ya changamoto ambazo zinashughulikiwa na Kanisa nchini Nigeria.

Kabla na wakati wa mchakato wa uchaguzi mkuu nchini Nigeria, anasema Askofu mkuu Kaigama, kulikuwa na hofu kubwa kwamba, Nigeria ingesambaratika kutokana na mipasuko ya kidini pamoja na mashambulizi yaliyokuwa yanafanywa na Kikundi cha kigaidi cha Boko Haram, lakini walau uchaguzi mkuu umepita salama na wahusika wakakubali matokeo na sasa Nigeria inasonga mbele. Nigeria inahitaji mchakato wa mageuzi makubwa, kwa Serikali kupambana kufa na kupona dhidi ya rushwa na ufisadi unaoendelea kuitumbukiza nchi katika hali ya umaskini, mipasuko na ukosefu wa haki na amani.

Ni matumaini ya Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria kwamba, Rais Muhammadu Buhari ambaye kwa sasa amekwisha kukaa madarakani walao kwa mwaka mmoja, ataweza kutekeleza bila mzaha ahadi alizowapatia wananchi wa Nigeria hasa katika mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi, unaoendelea kukineemeesha Kikundi cha Kigaidi cha Boko Haram ndani na nje ya Nigeria. Bado kuna mipasuko na misigano ya kidini kati ya Wakristo na Waislam hasa Kasikazini mwa Nigeria ambako wanabaguliwa kana kwamba, wao si raia wa Nigeria.

Uhuru wa kuabudu unatolewa kwa kuangalia imani ya mtu kana kwamba, huu ndio utambulisho wa raia wa Nigeria. Si rahisi kabisa kwa Kanisa kujenga nyumba mpya za Ibada Kaskazini mwa Nigeria, ingawa waamini wa dini ya Kiislam wanavyo vibali vya ujenzi na wala hawana vikwazo vyovyote. Mfumo wa elimu usipokuwa makini, ukavurugwa kwa misimamo ya kidini na kisiasa, matokeo yake ni kujenga makundi ya vijana wenye misimamo mikali ya imani, hatari kwa ustawi na maendeleo ya wengi.

Kuna haja anasema Askofu mkuu Kaigama kwa Serikali kuu nchini Nigeria kuhakikisha kwamba, mfumo wa elimu haufungamani na sera za kidini kwani kufanya hivi ni kuhatarisha umoja wa kitaifa na mafungamano ya kijamii. Serikali ya Rais Buhari inaonesha kwamba, inataka kulivalia njuga suala la amani na utulivu kwa kuwashughulikia Boko Haram pasi na huruma.

Kumbe, mapambano yote haya yanaweza kupata mafanikio makubwa ikiwa kama wananchi watajenga mshikamano wa dhati na familia zitaendelea kujengewa uwezo wa kurithisha tunu msingi za maisha ya kiutu, kimaadili na kiroho ili kujenga taifa la wachamungu, watu wanaoheshimu na kuthamini Injili ya uhai badala ya kugubikwa na utamaduni wa kifo! Nchi ambayo watu wake wanaongozwa na kanuni maadili, utu wema na upendo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.