2016-07-14 14:24:00

Tuko mikononi mwa Mungu, mlinzi mkuu!


Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 13 Julai 2016 asubuhi amewatembelea na kuzungumza na wajumbe wa Tume ya Kipapa ya Amerika ya Kusini, waliokuwa wanafanya mkutano wao kama sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu huko Amerika ya Kusini yatakatoadhimishwa mjini Bogotà, nchini Colombia. Baba Mtakatifu alisalimiana na wajumbe na kuomba ridhaa yao ili aweze kushiriki pia katika mkutano wao kama mjumbe msikilizaji.

Professa Guzmàn Carriquiry, Katibu mkuu wa Tume ya Kipapa kwa ajili ya Amerika ya Kusini, alimpokea Baba Mtakatifu na kuzungumza naye kwa faragha kwa muda wa nusu saa hivi. Baba Mtakatifu ameshiriki mkutano huu kama mjumbe mwingine na wajumbe wakapata nafasi ya kupiga picha za kumbu kumbu katika tukio la nadra kama hili. Baba Mtakatifu alifanya matembezi haya baada ya kutoka kwenye matibabu ya jino kwenye Zahanati iliyoko ndani ya Vatican.

Baba Mtakatifu alionesha nia ya kutaka kutembelea Makao makuu ya Tume ya Kipapa kwa ajili ya Amerika ya Kusini, lakini akaambiwa na vyombo vya ulinzi na usalama kwamba, uwezekano huo ulikuwa ni mdogo kwa sababu ya usalama na protokali ambazo zinapaswa kuzingatiwa. Lakini, Baba Mtakatifu alimhakikishia mhusika wa ulinzi na usalama wa Papa kwamba, hakuna wasi wasi kwani wako mikononi mwa Mungu, kumbe hata bila kuzingatia protokali wangeweza kwenda.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.