2016-07-13 15:04:00

Maaskofu USA wapongeza uteuzi wa Dr. Greg & Dr. Paloma


Askofu mkuu Joseph E. Kurtz, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani anachukua fursa hii kumpongeza Dr. Greg Burke kwa kuteuliwa na Baba Mtakatifu Francisko kuwa Msemaji mkuu mpya wa Vatican. Anapenda kuchukua nafasi hii, kumshukuru na kumpongeza pia Padre Federico Lombardi ambaye amekuwa msemaji mkuu wa Vatican kwa kipindi cha miaka kumi.

Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani linasema, katika kipindi cha uongozi wake kama msemaji mkuu wa Vatican, Padre Lombardi amekuwa ni shuhuda na chombo cha Uinjilishaji sehemu mbali mbali za dunia kwa njia ya huduma kwa Papa mstaafu Benedikto XVI na Baba Mtakatifu Francisko. Padre Lombardi alionesha weledi mkubwa katika tasnia ya mawasiliano ya jamii, akawa shuhuda wa upendo kwa Kristo na Kanisa lake. Huu ni ushuhuda aliouona mwenyewe wakati Baba Mtakatifu Francisko alipotembelea nchini Marekani kunako mwaka 2015.

Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani linampongeza Dr. Greg Burke kwa kuteuliwa kwake kuwa Msemaji mkuu wa Vatican. Ni mwandishi wa habari anayefahamika sana miongoni mwa Maaskofu Katoliki Marekani kutokana na uchaji na ushupavu wake katika tasnia ya mawasiliano ya jamii. Kutokana na majitoleo na sadaka yake tangu alipoteuliwa kufanya kazi kwenye Sekretarieti kuu ya Vatican ameonesha kwamba, ni kiongozi anayewajibika barabara kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa la Kristo ulimwenguni.

Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani linampongeza pia Dr. Paloma Garcìa Ovejero kwa kuteuliwa kuwa Msemaji mkuu msaidizi wa Vatican na kwamba, huyu anakuwa ni mwanamke wa kwanza kushika madaraka makubwa namna hii katika tasnia ya habari mjini Vatican. Baraza la Maaskofu Katoliki linawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kutokana na huduma za Padre Lombardi, Greg na Paloma, ambao wanaitwa kushiriki huruma ya Mungu, ili waweze kuwa ni vyombo vya Uinjilishaji kwa wale watu wenye kiu na njaa ya kusikia Neno la Mungu katika maisha yao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.