2016-07-11 09:11:00

Yaliyojiri maadhimisho ya Kongamano la Ekaristi Takatifu Kitaifa, Mwanza!


Kristo ndani yenu tumaini letu la utukufu ndiyo kauli mbiu iliyoongoza maadhimisho ya Kongamano la Tatu la Ekaristi Takatifu Kitaifa nchini Tanzania lililofanyika Jimbo kuu la Mwanza, Tanzania kuanzia tarehe 9 hadi 11 Juni 2016 kwa kuwa na uwakilishi mkubwa wa familia ya Mungu kutoka katika Majimbo thelathini na tatu ya Kanisa Katoliki nchini Tanzania. Katika mahubiri yake kwenye Ibada ya ufunguzi, Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwaichi wa Jimbo kuu la Mwanza aliitaka familia ya Mungu nchini Tanzania kujisadaka ili kumpeleka Kristo kwa watu wasiomfahamu bado kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko.

Itakumbukwa kwamba, maadhimisho ya Kongamano la Ekaristi Takatifu Kitaifa nchini Tanzania yalikuwa ni mwendelezo wa maadhimisho ya Kongamano la 51 ya Ekaristi Takatifu kimataifa lililoadhimishwa Jimbo kuu la Cebu, nchini Ufilippini. Jimbo kuu la Mwanza lilikuwa ni mwenyeji ili kuenzi hija ya kitume iliyofanywa na Mtakatifu Yohane Paulo II nchini Tanzania kunako mwezi Septemba 1990. Maandamano ya Ekaristi Takatifu ni kuwawezesha waamini kumtembeza Kristo katika viunga vya maisha yao, ili aweze kuwabariki na kuwatakatifuza, ili kweli wawe ni vyombo na mashuhuda wa upendo kati ya watu wa mataifa!

Yesu Kristo ni mkombozi wa pekee wa ulimwengu; mkate kwa ajili ya uzima mpya; Ekaristi ni muungano na Kristo na sisi wenyewe. Hizi ni kauli mbiu ambazo zimeongoza maadhimisho ya Makongamano ya Ekaristi Takatifu Kitaifa yaliyofanyika Jimboni Dodoma na Iringa. Baada ya maadhimisho ya Kongamano la Ekaristi Takatifu Kitaifa, familia ya Mungu nchini Tanzania sasa inawajibikakusimamia na kushuhudia haki na ukweli; kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa na Ibada ya Kuabudu Sakramenti kuu.

Waamini wanahamasishwa kujenga na kudumisha utamaduni wa kusali, kutafakari na kumwilisha Neno la Mungu katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili, changamoto ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kwa kutambua kwamba, jina la Mungu ni huruma iliyofunuliwa kwa njia ya Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu! Hii ni changamoto kwa Kanisa la Tanzania kujisimika katika Ekaristi Takatifu, mkate unaomegwa na kutolewa sadaka kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi! Ili kufanikisha lengo hili, waamini hawana budi kujiandaa vyema kushiriki kikamilifu katika Fumbo la Ekaristi Takatifu kwa kupokea mara kwa mara Sakramenti ya Upatanisho.

Askofu Salutaris Melchior Libena wa Jimbo Katoliki Ifakara alipembua umuhimu wa maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu; historia ya mageuzi yaliyoletwa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican hadi nyakati hizi. Liturujia ya Neno, Liturujia ya Ekaristi, Ibada na uchaji wakati mwamini anapokuwa Kanisani kwa kutambua kwamba, Tabernakulo ni mahali ambapo Kristo Yesu yumo na kwamba, Altare ni kielelezo cha Kristo kuhani mkuu, Altare na Mwanakondoo wa Mungu anayeondoa dhambi za ulimwengu. Waamini washiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa kwa kutambua hatua mbali mbali, ili wanaporejea nyumbani waweze kuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu katika maisha ya watu kwa kumwilisha Ibada ya Misa Takatifu katika uhalisia wa maisha yao.

Padre Raymond Saba, Katibu mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania alipembua mada kuhusu Ekaristi na Uadilifu wa uumbaji, kwa kuwataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuthamini, kuendeleza na kutunza kazi ya uumbaji ambayo binadamu amekabidhiwa na Mwenyezi Mungu. Ekaristi Takatifu ni chanzo na kilele cha wito na maisha ya Kikristo. Baba Mtakatifu Francisko anawahamasisha waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kusimama kidete kulinda, kutunza na kuendeleza mazingira nyumba ya wote kwa kutambua athari ambazo zinaendelea kujitokeza katika uso wa dunia kutokana na uharibifu wa mazingira unaochangiwa kwa kiasi kikubwa na kazi ya binadamu.

Ikumbukwe kwamba, Ekaristi Takatifu inaunganisha mbingu na dunia; Sifa iwe kwako, juu ya utunzaji wa mazingira, Laudato si! Watu wanapaswa kuwajibika kwa kutunza mazingira kwani hii ni dhamana ya kimaadili na kiimani! Maisha ya kila siku yaoneshe ile furaha inayobubujika katika wito wa kila mwamini ndani ya Kanisa! Ekaristi takatifu ni chakula kinachowapatia waamini nguvu na ujasiri wa kuweza kusimama kidete hata kuyamimina maisha yao kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake.

Waamini wa  Kanisa la mwanzo walikuwa wanasema hawawezi kuishi bila maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, kwani humo walikuwa wanajichotea nguvu na hekima ya kimungu. Waamini watambue, waheshimu na kushiriki Ibada ya Misa Taktifu kwa uchaji na moyo mkuu, ili kweli waamini waweze kujimega na kujisadaka kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya familia ya Mungu. Waamini wawe makini katika matumizi ya chakula kwani uharibifu wa chakula ni sawa na kumwibia maskini haki yake!

Askofu Msaidizi Methodius Kilaini wa Jimbo Katoliki Bukoba aliwasilisha mada kuhusu Ekaristi Takatifu kama Utume wa waamini unaopata chimbuko lake baada ya waamini kushiriki Fumbo la Ekaristi Takatifu. Yesu Kristo aliwaonesha watu huruma na upendo wake na kwa njia hii akawaita na kuwapatia dhamana na wajibu wa kushiriki katika maisha na utume wake, kama ilivyokuwa kwa Simoni, Zakayo na Wafuasi wa Emmau. Yesu alitumia chakula kama njia na daraja la kuwaunganisha watu katika maisha na utume wake. Ekaristi ni nguvu ya kimissionari iliyowapatia ari na moyo wa kujisadaka kwa jili ya kutangaza Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia.

Wakristo wengi walikuwa tayari kukabiliana na kifodini baada ya kupokea Ekaristi Takatifu na kwamba, Ekaristi ni nguvu ya pekee katika mchakato wa Uinjilishaji. Hii ni changamoto kwa familia ya Mungu nchini Tanzania kuhakikisha kwamba, inashiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu kwa ari, moyo mkuu na uchaji.

Askofu Bernadin Mfumbusa wa Jimbo Katoliki Kondoa aliwasilisha mada juu ya majadiliano ya kiekumene na kidini kama njia ya kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani, upendo na maridhiano kati ya watu, kwa kuongozwa na kanuni ya dhahabu. Familia ya Mungu nchini Tanzania inapaswa kujikita katika mchakato wa majadiliano ya waamini wa dini na madhehebu mbali mbali ili kujenga na kuimarisha upendo, umoja na mshikamano wa kitaifa; tayari kushiriki katika huduma makini kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya watanzania wengi.

Ekaristi Takatifu na Vyama vya Kitume ni mada iliyopembuliwa na Padre Titus Amigu akiwataka waamini kuwa waaminifu kwa Kristo na Kanisa lake na kuacha mtindo wa kuhamahama kutafuta Makanisa na dini nyingine. Kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo waamini wanakaribishwa na kushirikisha maisha na utume wa Kristo, dhamana wanayopaswa kutolea ushuhuda wenye mvuto na mashiko; kwa kujichotea nguvu kutoka katika Sakramenti ya Ekaristi Takatifu.

Padre Amigu anakumbusha kwamba, Kanisa lina vitambulisho vikuu vitatu navyo ni: Kanuni ya Imani: Inayojikita kwa Utatu Mtakatifu; Kanisa na Mambo ya nyakati; Sakramenti Saba za Kanisa na Mamlaka ya Kanisa. Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ya Shukrani inayowakumbusha waamini kwamba, wanahitajiana na kukamilishana katika hija ya maisha yao hapa duniani. Waamini wametakiwa kuwa imara na thabiti katika imani yao na kamwe wasiyumbishwe na imani za kishirikina.

Vyama vya Kitume ndani ya Kanisa vinapaswa kuwa ni vyombo vya shuhuda za kiimani na Uinjilishaji kwa kuwa na umoja na Kanisa pamoja na kufuata sheria na kanuni za Kanisa ili kujenga na kudumisha amani na utulivu; Upendo na mshikamano. Vyama vya kitume vijenge utamaduni wa kuboresha maisha na utume wake kwa kupokea wanachama wapya mara kwa mara. Parokia zivisaidie vyama vya kitume na kwamba, vyama hivi vijenga maisha na utume wake kuzunguka Ekaristi Takatifu kama kiini cha Ukatoliki wao.

Ekaristi Takatifu na Sakramenti ya Upatanisho ni tema iliyopembuliwa kwa kina na mapana na Askofu Liberatus Sangu wa Jimbo Katoliki Shinyanga kwa kusema kwamba, Ekaristi ni chanzo cha maisha na utume wa Kanisa na hakuna Kanisa pasi na Ekaristi. Ekaristi Takatifu inawaimarishia waamini namna yao ya kufikiri na kutenda na kwamba, Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na Upatanisho ni Sakramenti pacha zinategemeana na kukamilishana katika maisha na utume wa waamini. Familia ya Mungu nchini Tanzania inahamasishwa kujenga utamaduni wa kuabudu Ekaristi Takatifu na kwamba, Mapadre wawe kweli sadaka kwa ajili ya kuwagawia waamini huruma ya Mungu inayopata chimbuko lake katika Sakramenti ya Upatanisho.

Ikumbukwe kwamba, uhai wa maisha ya Parokia unapimwa na idadi ya waamini wanaoungama dhambi zao na wala si idadi ya waamini wanaopokea Ekaristi Takatifu kwa mazoea. Waamini wachunguze dhambi zao, wafanye toba na majuto ya kweli; waziungame na hatimaye kufanya malipizi ya kweli. Malipizi yanaganga na kuponya madonda ya dhambi na madhara yake. Mapadre wanakumbushwa umuhimu wa kuwahimiza waamini wao kupokea Sakramenti ya Upatanisho, lakini wao wenyewe wakionesha pia mfano kwamba wanapaswa kuonja na kupokea huruma ya Mungu ili wawe kweli ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu kwa watu wake.

Askofu Ludovick Minde wa Jimbo Katoliki Kahama, alipembua kuhusu Ekaristi Takatifu, Bikira Maria na Familia kwa kusema kwamba, Bikira Maria ni Tabernakulo ya kwanza ya Neno wa Mungu aliyefanyika mwili. Bikira Maria ni mwanamke wa Ekaristi na kwamba Kanisa linapata uzima wake kwa njia ya Ekaristi Takatifu. Bikira Maria ni kama Eva mpya, ni Mama wa Mungu na Kanisa. Ni Mama aliyewazawadia walimwengu Ekaristi Takatifu. Familia ya Mungu nchini Tanzania inahamasishwa kujenga na kuimarisha misingi bora ya familia, kwa kuiga mfano wa Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu. Kristo Yesu alipokuwa anaweka Ekaristi Takatifu Bikira Maria alishuhudia, lakini hakuchaguliwa kuwa mwadhimishaji bali dhamana hii Yesu aliwapatia mitume wake kufanya hivyo kwa ajili ya ukumbusho wake. Waamini wajifunze kuwa ni watu washukrani kwa kumuiga Bikira Maria katika utenzi wake wa Magnificat, unaojikita katika unyenyekevu na ukuu wa Mungu katika maisha ya mwanadamu!

Makala haya yameandaliwa na Donesta Byarugaba, Makamu Mwenyekiti Halmashauri Walei Jimbo kuu la Dar es Salaam na kuhaririwa na

Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.