2016-07-09 07:53:00

Umoja wa Afrika, kumekucha, Kigali, Rwanda!


Umoja wa Afrika unatarajia kuanza mkutano wake mkuu wa 27 utakaofanyika mjini Kigali, Rwanda kuanzia tarehe 10 - 18 Julai 2016 kwa kuongozwa na kauli mbiu “2016: Mwaka wa Haki Msingi za Binadamu Barani Afrika, Mkazo ni Haki za Wanawake”.  Dr. Nkosazana Dlamini Zuma, Kamishina wa Umoja wa Afrika unaounganisha nchi 54 za Kiafrika anatarajiwa kumaliza muda wake wa uongozi na hatarajii kuomba tena kuongoza awamu ya pili, anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema Barani Afrika kusali ili kuombea mafanikio katika mkutano wa Umoja wa Afrika.

Familia ya Mungu nchini Ethiopia kwa mwaliko kutoka kwa Kardinali Berhaneyesus Souraphiel, Rais wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki, AMECEA kuanzia tarehe 1 Julai hadi tarehe 9 Julai 2016 wanasali Novena kwa ajili ya kuombea mafanikio ya mkutano wa 27 wa Umoja wa Afrika, ili Afrika iweze kupata mafanikio, maendeleo na kudumisha amani, umoja, mshikamano na udugu. Kardinali Souraphiel anaitaka pia Familia ya Mungu kutoka katika Nchi za AMECEA kujiunga katika sala kwa ajili ya kuombea mafanikio ya Umoja wa Afrika.

Hiki ni kipindi kigumu kwa Umoja wa Afrika kwani viongozi wakuu wan chi watapaswa kuchagua Mwenyekiti mpya wa Kamishina wa Umoja wa Afrika pamoja na Tume nyingine za Umoja wa Afrika. Umoja wa Afrika umekuwa mstari wa mbele chini ya uongozi wa DR. Zuma kuhamasisha maendeleo ya endelevu, demokrasia na utawala wa sharia kadiri ya Katiba na mwongozo wa Umoja wa Afrika.

Bara la Afrika kwa sasa linakabiliwa na changamoto kubwa ya haki, amani, usalama na utulivu mambo ambayo yalipewa pia kipaumbele cha pekee na Umoja wa Afrika kuanzia mwaka 2012. Usalama wa chakula, rasilimali , elimu, afya, biashara na ushirikiano wa kimataifa ni mambo ambayo yanaendelea kufanyiwa kazi. Kwa sasa majina yanayozunguka kwenye mitandao ya kijamii ya Umoja wa Afrika kuwania nafasi ya uongozi ni pamoja na Dr. Pelomoni Venson- Moitoi kutoka Botswana, DR. Speziosa Naigaga Wandira Kazibwe kutoka Uganda na Agapito Mba Mokuy kutoka Equatorial Guinea. Morocco ni nchi ya pekee Barani Afrika ambayo si mwanachama wa Umoja wa Afrika ingawa ni mwanachama wa Umoja wa Mataifa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.