2016-07-09 09:38:00

Mapadre wawe ni chemchemi ya baraka na neema!


Mapadri wameshauriwa na  kukumbushwa kuwa kazi yao kuu waliyoitiwa kuifanya ni kubariki na kwamba kamwe vinywa vyao visitoe laana kwa watu wanaitiwa kuwahudumia. Ushauri huo umetolewa na Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam wakati wa ibada ya Misa takatifu ya kuwekwa wakfu Mapadri wapya watatu wa Jimbo wa Jimbo Kuu Dar es Salaam iliyoadhimishwa tarehe 7 Julai 2016 katika Parokia ya Mt. Petro Oysterbay. Ibada hiyo ya Misa takatifu iliongozwa na Askofu Msaidizi Eusebius Nzigilwa wa Jimbo kuu la Dar es Salaam.

Akizungumza baada ya kuwakabidhi majukumu Mapadre hao wapya na kuwabadilishia Mapadre wengine vituo vya kazi,  Kardinali Pengo amesema katika kinywa cha Padri patoke baraka na maneno yakufariji  waamini na kwa watu wengine wote kwa ujumala. “Mnapaswa kuwabariki waamini kwa maneno yenu na kamwe lisitoke neno la laana kutoka kinywani mwenu”, Amesema Kardinali Pengo. Aidha amewahimiza waamini kutoamini hata siku moja Padri akiinuka na kuaanza kuwaambia kuwa atawalaani kwani Padri hakutumwa kwa kazi ya kulaani bali kubariki. Amesema endapo Padri anataka kuwalaani waamini afanye hivyo kwake (Kardinali) ambapo amesema kwa misingi ya Kanisa yupo tayari kulaaniwa kuliko kubadilisha mfumo wowote katika Kanisa Katoliki.

Naye Askofumsaidizi Eusebius Nzigilwa wa Jimbo kuu la Dar es Salaam akitoa mahubiri kwa Mashemasi hao watatu ambao sasa ni Mapadri wapya amesema, pamoja na mambo mengine wanatumwa kuwavua watu kutoka katika himaya inayotwaliwa na shetani na kuwaingiza katika himaya ya Mungu. Amesema wanapaswa kufanya utume wao katika kuwatoa watu wa Mungu katika mazingira yanayohatarisha usalama wa uzima wao na kuwaweka katika mazingira salama. Amesema watafanikiwa katika hilo kupitia kutoa huduma ya Neno la Mungu na huduma ya Sakramenti kwani Neno la Mungu na Sakramenti ndiyo yanayoleta uzima mpya katika mioyo ya waamini.

“Ili ninyi kuwatoa watu katika hilo dimbwi la maangamizi na minyororo ya ibilisi lazima mkawahubirie watu kwa maneno na matendo yenu na mkawahudumie kisakramenti na zaidi sana Sakramenti ya Ekaristi na kitubio” amesema Askofu Nzingilwa Aidha amewaambia waamini kuwa bila kulitafakari Neno la Mungu hawawezi kuwa na mwanga wa kuongoza maisha yao na hawawezi kujua Mungu anataka nini ili waweze kufika mbinguni. “…Neno la Mungu linatupatia mwongozo na kanuni zote za msingi zitakazotuwezesha sisi  kuishi vizuri na hatimaye kuupata uzima wa milele” amesema na kuongeza nikiona muumini hapokei masakramenti, Kanisani haendi na jumuiya haendi naona umejimaliza mwenyewe hata kama unatembea hauna uzima wa kimungu ndani yako.

Mashemasi watatu wa Jimbo la Dar es Salaam ambao wamewekwa wakfu na kuwa Mapadri ni pamoja na Padri James Ngonyani ametumwa kuwa Paroko Msaidizi wa Parokia mpya ya Wazo Hill, Padri William Sindano  ambaye ametumwa kuwa Paroko msaidizi katika Parokia ya Kizinga na Padri Francisco Jose  ambaye ametumwa kuendelea na masomo yake ya juu huko Nchi Takatifu. Wakati wa salamu zake hizo Kardinali Pengo alizitangaza rasmi Parokia mpya tano na kufanya idadi ya Parokia katika Jimbo hilo kufikia mia moja. Parokia hizo mpya ni Parokia ya Wazo Hill, Parokia ya Tabata Kisiwani, Parokia ya Magole, Parokia ya Mbagala Kuu na Parokia ya Mikoroshoni.

Imeandaliwa na Padre Joseph Peter Mosha, Roma – Italia.








All the contents on this site are copyrighted ©.