2016-07-09 13:24:00

Askofu mkuu Franco Coppola ateuliwa kuwa Balozi nchini Mexico


Baba Mtakatifu Francisko amemteua Askofu mkuu Franco Coppola kuwa Balozi mpya wa Vatican nchini Mexico, kabla ya uteuzi huu, Askofu mkuu Coppola alikuwa ni Balozi wa Vatican Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati aliyeshiriki kuandaa hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Afrika ya Kati, tukio ambalo limeacha chapa ya kudumu kwa familia ya Mungu nchini humo, kwani Baba Mtakatifu Francisko akiwa Jimbo kuu la Bangui aliweza kufungua Lango la Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kwa mara ya kwanza katika historia ya Kanisa, tukio kama hili kufanyika nje ya Vatican.

Askofu mkuu Franco Coppola alizaliwa kunako tarehe 31 Machi 1957 huko Maglie, Italia. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, kunako tarehe 12 Septemba 1981 akapewa Daraja Takatifu la Upadre. Kunako mwaka 1993 akajiunga na utume wa Kidiplomasia mjini Vatican na kubahatika kufanya utume wake nchini Lebanon, Burundi, Colombia, Poland na hatimaye Vatican. Tarehe 16 Julai 2009 Papa mstaafu Benedikto XVI akamteuwa kuwa Askofu mkuu na hatimaye kumweka wakfu kuwa Askofu hapo tarehe 12 Septemba 2009. Tangu wakati huo amekuwa ni Balozi wa Vatican nchini Burundi, Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati na Chad. Tarehe 9 Julai 2016 ameteuliwa na Baba Mtakatifu Francisko kuwa Balozi mpya wa Vatican nchini Mexico.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.