2016-07-06 08:04:00

Barua ya Kichungaji Baraza la Maaskofu Katoliki Afrika ya Kusini!


Baraza la Maaskofu Katoliki Afrika ya Kusini limewaandikia waamini na watu wote wenye mapenzi mema barua ya kichungaji inayoongozwa na kauli mbiu “Basi, ndugu zangu, nawasihi, kwa huruma zake Mungu… mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate kujua hakika mapenzi ya Mungu yaliyo mema, ya kumpendeza na ukamilifu” (Rej. Rum. 12: 1-2). Lengo la barua hii ya kichungaji ni kuwasaidia waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa jamii kwa njia ya demokrasia itakayowawezesha kupata viongozi makini kwa ajili ya maendeleo ya wengi.

Baraza la Maaskofu Katoliki Afrika ya Kusini linasema, Jamii inahitaji viongozi wenye nidhamu, watakaowajibika barabara kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi; wagunduzi na wachapa kazi watakaosaidia upatikanaji wa fursa za ajira na maboresho ya maisha ya wananchi wengi wa Afrika ya Kusini ambao kwa sasa wanaogelea katika dimbwi la umaskini na huduma hafifu za kijamii. Jamii inahitaji viongozi wabunifu watakaopambana na hali ngumu ya kiuchumi, ili kuwajengea wananchi uwezo wa kujiletea wenyewe maendeleo.

Jamii haina haja na viongozi wenye uchu wa mali na madaraka; wapambe wa vyama vyao vya kisiasa wasioguswa na mahangaiko ya wananchi wengi wa Afrika ya Kusini. Kwa waamini, siasa ni wito unaopaswa kutekelezwa kwa ari na moyo mkuu, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa ustawi na maendeleo ya wengi! Baba Mtakatifu Francisko anasema, Jamii zinawahitaji viongozi watakaojitosa kimasomaso bila ya kujibakiza kwa ajili ya kuwasaidia maskini kuondokana na umaskini wao.

Falsafa ya uongozi ijikite katika huduma makini kwa familia ya Mungu nchini Afrika ya Kusini badala ya kishawishi cha uchu wa mali na madaraka na matokeo yake ni rushwa na ufisadi wa mali ya umma pamoja na kushindwa kutekeleza mafao ya wengi. Ni wajibu wa familia ya Mungu nchini Afrika ya Kusini kuhakikisha kwamba, inawachagua viongozi wanaojipambanua kwa maadili na utu wema; watu ambao wako tayari kusimamia utawala wa sheria; wakweli na waaminifu; wattu watakaowajibika kwa ajili ya huduma makini kwa maskini na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Baraza la Maaskofu Katoliki Afrika ya Kusini linaitaka familia ya Mungu kutumia kura yake kwa ajili ya kukuza na kudumisha mafao ya wengi na kwa ajili ya kuboresha huduma kwa jamii. Waangalie ikiwa kama wanasiasa hawa waliweza kutekekeza ahadi zao na ikiwa kweli Jamii inaridhika na huduma za viongozi waliko madarakani katika mchakato wa mapambano dhidi ya rushwa na ubadhilifu wa mali ya umma. Maaskofu wanawataka wananchi kuhakikisha kwamba, wanadumisha misingi ya haki, amani na utulivu ili kuwezesha uchaguzi kuwa huru na wa haki. Huu ni wajibu unaopaswa pia kutekelezwa na wanasiasa na vyombo vya upashanaji habari nchini Afrika ya Kusini.

Maaskofu wanawataka wanasiasa kuachana na kampeni za uchochezi na matusi; mambo ambayo hayana tija wala mashiko kwa ustawi wa maendeleo ya wananchi wa Afrika ya Kusini. Vyombo vya ulinzi na usalama viwe makini kuwathibiti wanasiasa na wapambe wao watakaoleta vurugu wakati wa mchakato wa uchaguzi mkuu na kwamba, vyama vyote vinapaswa kuheshimu matokeo ya uchaguzi na kwamba, utawala wa sheria unapaswa pia kuzingatiwa na wote. Vyombo vya habari viwe makini wakati wote wa uchaguzi ili kudumisha mafao ya wengi.

Wananchi wanapotekeleza dhamana na wajibu wao wasichoke kumkimbilia Mungu kwa njia ya sala, ili aweze kuwapatia viongozi: watakaohudumia kwa haki, upendo na huruma, daima wakimtegemea Mungu katika maisha yao. Wawe ni viongozi watakaojitosa kwa ajili ya mafao ya wengi badala ya kujitafuta mwenyewe! Barua ya kichungaji ya Baraza la Maaskofu Katoliki Afrika ya Kusini imetiwa mkwaju na Askofu mkuu William Slattery., OFM.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.