2016-07-02 15:49:00

Mapadre wapya angalieni msimezwe na malimwengu!


Mama Kanisa anatoa Daraja Takatifu la Upadre ili kuwaingiza Mashemasi katika Ukuhani wa Kristo na hatimaye, kuwaweka wakfu ili kushiriki kikamilifu katika kufundisha Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa mataifa; kuwatakatifuza watu wa Mungu kwa njia ya sala, sadaka na Sakramenti za Kanisa pamoja na ushuhuda wa maisha na wito wa kipadre, kielelezo cha imani tendaji. Mapadre wanawekwa wakfu ili kuongoza kundi la Kristo mchungaji mwema, aliyemimina maisha yake Msalabani kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi la mauti!

Mashemasi kabla ya kuwekwa wakfu kuwa Mapadre wanakula kiapo cha useja mbele ya Askofu Mahalia. Huu ni uamuzi unofanywa na watu wazima kwa kutambua kwamba, sasa wanakuwa ni Mababa wa familia ya Mungu, jambo ambalo ni heshima kubwa na wajibu unaowataka kuchakarika usiku na mchana kwa ajili ya kuwahudumia watu wa Mungu kwa kuhakikisha kwamba, wanapata huduma makini zinazotolewa na Mama Kanisa.

Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwaichi wa Jimbo kuu la Mwanza wakati wa Maadhimisho ya Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo, miamba wa imani, hapo tarehe 29 Juni 2016 sanjari na kutoa Daraja Takatifu la Upadre kwa Mashemasi sita kutoka Jimbo Kuu la Mwanza. Katika wosia wake, amewataka Mapadre wapya walioamua kujongea mbele na kupewa Daraja Takatifu la Upadre kwa uhuru kamili, uelewa na ukomavu kuhakikisha kwamba, wanakuwa shupavu katika maisha na utume wao na kamwe wasirudi nyuma.

Kamwe Mapadre wapya wasikengeuke, kwani watu watawashangaa na kuwadharau. Kama Askofu na Baba atajitahidi kuwasaidia kwa moyo wote, lakini pale itakaposhindikana atawashughulikia kikamilifu. Askofu mkuu Ruwaichi anawataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuwasindikiza Mapadre wapya kwa njia ya sala, kwani ni watu wanaowekwa wakfu katika zama za usasa na ulimwengu mamboleo. Mapadre anaitwa kuyatakatifuza malimwengu na kamwe wasiburuzwe na malimwengu haya kwani huko watakiona kilichomnyoa Kanga manyoya! Wayatolee maisha yao kwa ajili ya ulimwengu pasi na woga wala makunyanzi. Paulo mtume na mzee aliyeitikia wito wa Kristo akapiga vita kumtangaza na kumshuhudia kwa watu wa Mataifa bila kuchoka, mwishoni anamshukuru Mungu na kumwomba amkirimia taji ya ushindi.

Askofu mkuu Ruwaichi anawataka Mapadre kujenga utamaduni wa kuchuguza dhamiri zao kila siku na kuangalia jinsi ambavyo wanamfuasa Kristo Yesu katika maisha na utume wao. Waangalie jinsi ambavyo wanatoa huduma kwa familia ya Mungu, watambue kwamba, kuna vigingi mbele yao, lakini wanapaswa kuwa shupavu. Askofu mkuu Ruwaichi, kama wosia wake kwa Mapadre wapya ni  kuwataka kujitahidi kuangalia jinsi ambavyo wanaishi wito wao wa Kipadre na wala si wingi wa miaka. Kwani kuna watu ambao wameadhimisha Jubilei ya miaka 50 ya Upadre, Miaka 35, Miaka 25 na wengine ndio kwanza kabisa wako kwenye nyumba za malezi. Mapadre wapya ni: Pd. John Kasembo kutoka Parokia ya Igoma, Pd. Sumira Vesuini, Parokia ya Sumve, Pd. Daniel Kadogosa, Parokia ya Kahangara, Pd. Stefano Bikoramungu, Parokia ya Buzurugwa, Pd. Kelvin Mkama, Parokia ya Mabatini pamona na Pd. Stefano F. Karabyo, C.PP.S, Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu, Kanda ya Tanzania.

Na Rodrick Minja na kuhaririwa na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.