2016-07-01 16:12:00

Msithubutu kuchezea amani!


Askofu Abel Gabuza wa Jimbo Katoliki la Kimberly, Afrika ya Kusini amewataka wananchi wa Afrika ya Kusini kutofanya mzaha na misingi ya haki, amani, usalama na mafao ya wengi na kwamba, wanawajibika barabara katika kukuza na kudumisha demokrasia ya kweli nchini Afrika ya Kusini. Askofu Gabuza anawataka wanasiasa na wapambe wao kutothubutu kuchezea amani na utulivu vinavyoendelea kushamiri kwa sasa nchini Afrika ya Kusini licha ya changamoto zilizopo!

Ili kukuza na kudumisha amani kuna haja kwa wananchi wote kuendelea kuwajibika barabara na kwamba, viongozi wa kisiasa wanapaswa kuonesha ukomavu wa kisiasa na kidemokrasia hasa wakati wa mchakato wa uchaguzi mkuu, yaani wakati wa kampeni, uchaguzi na utangazaji wa matokeo, kipindi hatari sana kinachoweza kulitumbukiza taifa katika maafa makubwa na hivyo misingi ya haki, amani, usalama na mafao ya wengi kutoweka kama ndoto ya mchana!

Askofu Gabuza ambaye ni Mwenyekiti wa Tume ya Haki na Amani Baraza la Maaskofu Katoliki Afrika ya Kusini anakaza kusema, hali ya matumizi ya nguvu, lugha chafu na uvunjifu wa sheria ni dalili kwamba, wanasiasa pamoja na wapambe wao wameshindwa kuwajibika barabara katika kulinda na kudumisha haki, amani na demokrasia ya kweli. Mchakato wa uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika nchini Afrika ya Kusini hapo tarehe 3 Agosti 2016 iwe ni fursa ya kushuhudia ukomavu wa kisiasa na uongozi bora unaopania ustawi na maendeleo ya wananchi wote wa Afrika ya Kusini.

Vyama vya kisiasa vinapaswa kuwadhibiti wanachama na wapambe wao, ili kujenga mazingira ya uchaguzi huru na wa haki. Malumbano na mapigano wakati wa maandamano ya vyama vya kisiasa ni hatari kwa umoja na mafungamano ya wananchi wa Afrika ya Kusini katika ujumla wao. Ni hatari sana kuendelea kuwatumia vijana kwa ajili ya kujijenga kisiasa na kwamba, vijana wasikubali hata kidogo kutumiwa na wanasiasa uchwara kuvuruga misingi ya haki, amani na umoja wa kitaifa nchini Afrika ya Kusini. Hawa ni viongozi wenye uchu wa mali na madaraka na watakapopata madaraka hawatawakumbuka hata kidogo. Askofu Abel Gabuza kwa namna ya pekee, anawaalika wananchi wa Afrika ya Kusini wenye sifa za kupiga na kupigiwa kura kujitokeza ili kutekeleza dhamana na wajibu wao wa kiraia kwa ajili ya ujenzi wa nchi yao na ukuzaji wa demokrasia na utawala bora!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 








All the contents on this site are copyrighted ©.