2016-06-28 15:35:00

Wakleri mnatumwa kutangaza na kushuhudia huruma na upendo!


Kardinali Gerhard Muller anasema Maadhimisho ya Kumbu kumbu ya miaka 65 ya Daraja Takatifu la Upadre kwa Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI ni fursa ya kupyaisha tena moyo wa huruma ya Mungu, ili hatimaye, waamini waweze kuguswa kwa namna ya pekee na huruma ya Mungu katika maisha yao kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Wakleri wanahamasishwa na kutumwa na Mama Kanisa kutangaza na kushuhudia Injili ya furaha, kwa kuwaondolea watu dhambi zao na kuwapatanisha na Mungu.

Kutangaza na furaha ni mambo makuu mawili yanayofumbwa katika Injili ambayo kwa sasa inashuhudiwa kwa namna ya pekee na Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake. Papa Mstaafu Benedikto XVI katika maisha na utume wake aliitaka familia ya Mungu kuwa na furaha kwa kujiaminisha na kujiachilia kwenye Fumbo na mpango wa Mungu. Furaha ya Injili ni zawadi inayobubujika kutoka katika Moyo Mtakatifu wa Yesu, uliomwonea mwanadamu huruma na mapendo; moyo ambayo unaweza kupyaisha maisha kutokana na Upendo wa milele.

Upendo huu ndio kichwa cha kitabu ambacho Mfuko wa Joseph Ratzinger unapenda kumzawadia Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI wakati huu anapoadhimisha Kumbu kumbu ya Miaka 65 ya Daraja Takatifu la Upadre. Ni kitabu ambacho kinafundisha na kujifunza Upendo wa Mungu, kwani kama Wakleri wanatumwa kufundisha kile ambacho wamepokea kutoka kwa Mwenyezi Mungu; Upendo ambao Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI ameifundisha familia ya Mungu kama Padre pamoja na Kaka yake Monsinyo Georg, wakati walipopewa Daraja Takatifu la Upadre, Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo, miamba wa imani.

Mapadre wanaitwa na kutumwa kutangaza Habari Njema ya Wokovu, dhamana iliyotekelezwa na Mtakatifu Paulo; wanahamasishwa kuwaimarisha ndugu zao katika imani, utume uliofanywa na Mtakatifu Petro. Kanisa linamshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI kwa Daraja Takatifu la Upadre.

Kwa upande wake, Kardinali Angelo Sodano, Dekano wa Makardinali amempongeza Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI kwa Daraja Takatifu la Upadre, Uaskofu na hatimaye kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Kwa niaba ya Makardinali wote, anamtakia heri na baraka na kwamba, wanajisikia kuwa na furaha ya ndani inayofumbatwa katika udugu na mshikamano wa huduma kwa Kanisa la Kristo. Hii ni huduma ambayo Wakleri wanapaswa kutambua kwamba, wanasindikizwa na umati mkubwa wa Watakatifu na waamini kwani wao ni marafiki wapendwa wa Kristo Yesu.

Wanaitwa na kutumwa ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Wakleri leo hii wanapaswa kuwa ni wajumbe wa mwanga na upendo wa Mungu kwa watu wake, kwa kuonesha upendo na mshikamano kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Huu ndio ujumbe unaopaswa kumwilishwa wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha Jubilei ya Mwaka Mtakatifu wa huruma ya Mungu. Ni muda muafaka wa kumshukuru Mungu kwa zawadi ya Daraja Takiatifu la Upadre kwa namna ya pekee wakati huu Papa mstaafu Benedikto XVI anapopanda Mlimani ili kusali na kutafakari kadiri ya nguvu na umri wake. Baba Mtakatifu Francisko ataendelea kulipyaisha Kanisa katika hija ya historia yake kwa ajili ya huduma kwa Jumuiya ya Kikristo na Ulimwengu katika ujumla wake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.