2016-06-24 08:28:00

Maendeleo ya kweli yazingatie utu na heshima ya binadamu!


Mchakato wa utandawazi umesaidia kwa kiasi kikubwa kukuza maendeleo ya binadamu katika medani mbali mbali za maisha, hali ambayo wakati mwingine imechangia kuvunjwa kwa haki msingi za binadamu, changamoto inayotolewa na mashirika na makampuni makubwa ya kimataifa katika sekta ya uzalishaji na utoaji wa huduma. Sheria ya kimataifa imeshindwa kudhibiti wimbi kubwa la uvunjifu wa haki msingi za binadamu kiasi hata kushindwa kutoa mbinu za kupambana na hali hii katika masuala ya haki msingi za binadamu.

Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Askofu mkuu Ivan Jurkovic, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Ofisi za Umoja wa Mataifa zilizoko mjini Geneva wakati akichangia mada kuhusu haki msingi za binadamu, wakati mkutano wa thelathini na mbili wa haki msingi za binadamu. Ujumbe wa Vatican unaupongeza Umoja wa Mataifa kwa kuchapisha Mwongozo wa masuala ya biashara na haki msingi za binadamu: “Linda, Heshimu na Rekebisha”. Kanuni hizi msingi zimeridhiwa na wengi lakini kuna haja ya kuongeza bidii zaidi ili kuweza kupata mafanikio yanayokusudiwa.

Sheria ya Kimataifa ni muhimu sana katika mchakato wa udhibiti wa Mashirika ya kimataifa yanayowekeana mikataba na Serikali mbali mbali katika shughuli za uwezekaji; mikataba ambayo wakati mwingine haizingatii haki msingi za binadamu. Kumbe, sheria ya kimataifa inapaswa kutekelezwa ili kuhakikisha kwamba, sheria na kanuni msingi zimezingatiwa kikamilifu. Hapa mkazo ni kusimama kidete kulinda haki msingi za binadamu zinazofumbata utu wa binadamu; uhuru pamoja na ushiriki wa wadau wengi katika masuala ya kisiasa ili kudumisha haki msingi za binadamu.

Utekelezaji wa haki msingi za binadamu ni changamoto pevu inayopaswa kujikita katika uwajibikaji pamoja na kuwashughulia wahusika kikamilifu. Wadau katika masuala ya biashara na uchumi wa kimataifa wanapaswa kuhusishwa, ili kusaidia mchakato wa maendeleo endelevu kwa binadamu kwa kujikita katika mshikamano unaofumbatwa katika matumizi na ugawaji bora zaidi wa rasilimali za dunia, ili kukuza na kudumisha mwingiliano wa watu.

Askofu mkuu Ivan Jurkovic anahitimisha mchango wa Vatican kwa kusema, mchakato wa maendeleo unapaswa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu na heshima ya binadamu badala ya fedha na faida kubwa; mambo ambayo yanachangia kudhalilishwa kwa utu na heshima ya binadamu pamoja na uvunjifu mkubwa wa haki msingi za binadamu. Ustawi, maendeleo na mafao ya wengi yapewe msukumo wa pekee ili kuonesha upendo na mshikamano kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Wadau mbali mbali wa mchakato wa maendeleo wasaidie kutoa fursa za maendeleo endelevu kwa watu ili kuweza kuchangia maendeleo yao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.