2016-06-22 11:23:00

Unaitwa kutangaza na kushuhudia huruma ya Mungu!


Ndugu msikilizaji, Dominika ya 13 ya Mwaka C wa Kanisa inatuletea sauti inayoita ikisema “Nifuate!”. Sauti hii ni ya Mungu ambaye anamuita kila mmoja wetu kwa nafasi yake ili kutekeleza jambo mahsusi kadiri ya mpango wa Mwenyezi Mungu. Huu ni wito wa kuufanya uwepo wa Mungu, uliofunuliwa kwetu kwa namna ya juu kabisa na Bwana wetu Yesu Kristo, kuendelea kuonjwa na na kila mwanadamu na kwa ufupi ni utekelezaji wa wito aliotupatia Kristo akisema: “mtapokea nguvu, akisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu, nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi” (Mdo 1:8). Hivyo wito huo wa Mungu ni mwaliko kwetu wa kuwa wajumbe au watumishi wake wa kuieneza huruma yake kwa wanadamu wote.

Neno la Mungu katika Dominika hii, hususani somo la Kwanza na somo la Injili linatuwekea mbele yetu muktadha huo wa kuitwa. Sehemu hii ya Maandiko matakatifu inatuonesha masharti ya kuitikia wito huo na pia tunaonywa juu ya hali na mazingira tutakayokabiliana nayo katika kutimiza majukumu tunayopewa na wito huo wa Mungu. Kwa nafasi ya kwanza tunaona kwamba wito wa Mungu unapotujia mwitikio wetu wa kwanza ni kuukubali wito huo bila kuweka masharti yoyote. Nabii Elisha anaonesha mfano huo wa kumpatia Mwenyezi Mungu nafasi ya kwanza. “Eliya akapita karibu naye, akatupa vazi lake juu yake. Nawe akawaacha ng’ombe, akamfuata Eliya mbio, akasema, Nipe ruhusa, nakuomba, nimbusu baba yangu na mama yangu, kisha mimi nitakufuata”.

Tofauti ya Elisha na Vijana wawili tunaowasikia katika somo la Injili ni namna ambavyo ruhusa imeombwa na hapo ndipo tunaona ni nini kipao mbele cha makundi haya mawili na namna gani kinatofautisha namna ya kuitikia wito. Elisha anasema “nipe ruhusa nakuomba” tena anasema hivi baada ya kuacha alichokuwa anakifanya na kumfuata Nabii Eliya. Huu ni uthibitisho wa utayari wa kutumikia. Yeye anakubali kwanza bila sharti lolote na hata hamu yake ya kwenda kuaga wazazi wake anaiweka katika namna ya ombi. Kwa kifupi kwake yeye Neno la Mungu ni kwanza na mengine yanafutia baadaye. Vijana wawili tunaowasikia katika somo la Injili mmoja anajibu akisema “Bwana, nipe ruhusa kwanza” na mwingine anasema “nitakufuata; lakini, nipe ruhusa kwanza”. Elisha aliomba ruhusa lakini hawa wanaitaka hiyo ruhusa kama sharti au kama jambo la kwanza kabla ya kuitikia wito. Hili linathibitishwa na matumizi ya maneno “nakuomba” kwa upande wa Elisha na “nipe” kwa upande wa vijana wa Injili.

Jambo la pili tunaloliona ni utayari wa kuacha yote ili kutumikia katika wito tunaoitiwa. Wengi huitikia wito wa Mungu bila kuwa tayari kuyaacha ya dunia ambayo huwa ni kikwazo katika kuisikia sauti ya Mungu. Hili linaunganika katika ugumu tulioutafakari hapo juu. Tunafungwa na ndugu zetu, mali zetu, vyeo vyetu na mengine mengi ya kidunia. Shughuli za kijamii kama mazishi na sherehe huwa yanatangulizwa kwanza kabla ya kuitikia wito wa sauti ya Mungu. Nabii Elisha kudhihirisha kuwa ameitikia kikamilifu Neno la Mungu linatuambia kwamba “akatwaa lile jozi la ng’ombe, akawachinja, akatokosa nyama zao kwa ile miti ya ng’ombe, akawapa watu, wakala. Kisha akainuka, akamfuata Eliya, Akamhudumia”. Hii ni ishara ya kuyaacha yote na kuwa tayari kwa utumishi. Yupo tayari kutumikia bila kufungwa na chochote cha kidunia kama vile mali, ambavyo huenda alikuwa ameviacha nyuma.

Kristo alipokuwa anamuonya yule kijana wa kwanza juu mazingira halisi ya utumishi anatuonya pia mimi na wewe kuwa hatuna budi kutambua kuwa wito huu unatudai kujisadaka zaidi na si katika kupata na kufarijika kibinadamu. Mwenyezi Mungu anapotuita katika wito huu wa kuwa vyombo vya kueneza upendo wake anatutaka kuwa tayari kuipoteza nafsi yetu kwa ajili ya Injili. Tusitegemee au tusiweke mbele kwanza mapato ya kijamii. Wito huu unaweza kukufanya kufika mahali ukakosa hata mahali pa kulala. Hii ni ishara ya kupoteza haki zako za msingi na hata hadhi yako ya kijamii kwa ajili ya Injili na kwa ajili ya upendo kwa jirani. Kristo mwenyewe anajiweka kama mfano kwamba “hana mahali pa kulaza kicha chake”. Huyu aliye Bwana wa ulimwengu na mmiliki wa vyote anajisadaka namna hii na ndipo anapokuita wewe na mimi kujisadaka namna hiyo.

Wito wetu mkuu tunaupokea kwa Sakramenti ya Ubatizo. Hii ni Sakramenti ambayo inatufanya kuwa watoto wa Mungu au kwa kutumia maneno ya Mtakatifu Augustino “tunafanywa kuwa Kristo”. Somo la pili linatuonesha hadhi tunayoipokea ya kuwa wana huru na hivyo kubaki katika hadhi hiyo bila kuipoteza kwa kufuata mwili. Na hivyo hadhi hiyo inatupa wito wa kuwa waeneza upendo kwa jirani. Hapa tunaona moja kwa moja umuhimu wa kuitikia wito wa Mungu kwa kadiri ya Neno lake. Pale tunapoanza kuitikia kama matamanio ya nafsi zetu yanavyotaka na si kama anavyotaka Mungu hapo tutaanza kudai ruhusa na si kuomba ili kuitikia wito huo. Hii inamaanisha kwamba tutapenda kujifungamanisha na malimwengu ambayo hayatupeleki katika kuufunua upendo wa Mungu bali ni kuendelea kutufanya wabinafsi na wasiotayari kujifunua na kujisadaka kwa ajili wa wengine.

Sehemu ya kwanza ya Injili ya leo inakwenda mbali zaidi kwa kutupatia wito mgumu kabisa ambao Kristo alikwisha udokeza katika hotuba yake ya mlimani aliposema “wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowahudhi” (Mt 5:44). Huu ni wito wa kuwatakia mema hata wale wanaokupinga au hata kuonesha kutojali upendo wako kwao. Hapa kwa hakika ndipo tunapoonja changamoto nzito wa kuwa wajumbe wa huruma ya Mungu kwa wengine. Mtu anayeukataa upendo wako bado unahamasishwa kutomlaani na kumtakia mema. Mitume Yakobo na Yohana wamejaa roho ya kisasi. Kwao wao wanaona kwamba kama wao wamemwaga mboga basi sisi tunamwaga ugali: “Bwana wataka tuagize moto ushuke kutoka mbinguni, uwaangamize?”. Maneno ya mtume Paulo, “lakini uhuru wenu usiwe sababu ya kuufuata mwili, bali tumikianeni katika upendo”, yanapata nafasi yake hapa. Uhuru katika Mungu umejaa upendo na si visasi, unanuia kujenga na si kuangamiza.

Mwanadamu peke yake bila kumpa Mungu kipaumbele anaona katika hali ya utumwa na kuutumikia mwili wake lakini kwa msaada wa neema ya Mungu anaendelea kupenda hata pale ukinzani unapokuwepo juu ya upendo huo. Huu ndio upendo wa kimungu na upendo huu unafupishwa zaidi katika historia nzima ya wokovu. Kwa maana “dhambi ilipozidi, neema ilikuwa nyingi zaidi (Rum 5:20). Mwenyezi Mungu ana upendo mkuu usio na kipimo. Yeye anaendelea kupenda bila kujali uhasi wa mwanadamu unaondelea. Yeye anampenda mwanadamu anayeathiriwa na dhambi na anaichukia dhambi ambayo inaufifisha upendo wake kwa mwanadamu. Huu ndiyo wito tunaoitiwa kwa kuwa wajumbe wa huruma ya Mungu, yaani kuwa tayari kumtafuta mwanadamu hata katika hali ya kudhalilika kiasi gani na kumfanya aionje tena huruma ya Mungu.

Tutafakari katika Dominika ya ya leo juu ya wito huu mahsusi na tumpatie mwenyezi Mungu nafasi ya kwanza ili ayatawale maisha yetu. Tujiepushe na mambo ya ulimwengu na tuwe tayari kujitoa kwa ajili ya wenzetu. Hapo ndipo tutakuwa kweli wahudumu wa huruma ya Mungu kwa watu wote.

Kutoka Studio za Radio Vatican mimi ni Padre Joseph Peter Mosha.








All the contents on this site are copyrighted ©.