2016-06-21 07:22:00

Malango wazi ya Kanisa kwa ajili ya huduma kwa maskini!


Kardinali Agostino Vallini, Makamu Askofu Jimbo kuu la Roma, hivi karibuni amemweka wakfu Askofu Msaidizi Gianrico Ruzza aliyeteuliwa hivi karibuni na Baba Mtakatifu Francisko kwa kumtaka awe ni chachu ya imani, matumaini na mapendo yanayoimarishwa na hatimaye kuzaa matunda ya utakatifu wa maisha. Askofu mpya anatumwa na Mama Kanisa kuwasaidia waamini kutamadunisha na kuimwilisha imani yao katika matendo. Katika maisha na utume wake, awe ni rejea na mwangaza angavu wa ushuhuda wa imani kwa Kristo na Kanisa lake.

Askofu msaidizi Ruzza amekumbushwa umuhimu wa huduma inayomwilishwa katika: Kufundisha, Kuongoza na Kuwatakatifuza watu wa Mungu katika hija ya maisha yao hapa duniani. Hapa Askofu Ruzza anapaswa kuonesha na kushuhudia upendo na ukarimu kwa familia ya Mungu Jimbo kuu la Roma na kwamba, dhamana yake uongozi kama Askofu iwe ni kielelezo wazi cha Kristo Mfufuka anayelijenga na kulitegemeza Kanisa lake katika imani na upendo.

Uwepo wake kama Askofu uwe ni kielelezo cha mwanga anagavu wa ukaribu wa Mungu kwa watu wake na rejea kwa wale wanaotaka kumwona Kristo katika mahangaiko yao ya ndani, ili aweze kuwaimarisha katika imani na kwamba, awe ni msaada mkubwa kwa Wakleri wenzake kwa kuwasikiliza kwa makini, kuwasaidia katika mahangaiko yao na kuwafariji kwa niaba ya Kanisa.

Baba Mtakatifu Francisko anawataka Maaskofu na viongozi wa Kanisa katika ujumla wao, kuhakikisha kwamba, wanajiasadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya waamini wale: kiroho na kimwili kwa kujikita katika majiundo makini na endelevu kama njia ya ujenzi wa Kanisa la Kristo. Jambo la mwisho, lakini muhimu kwa Askofu ni kuhakikisha kwamba, anatoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, ili waweze kuonja huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao.

Askofu Gianrico Ruzza ametakiwa pia kujisadaka kwa ajili ya utume kwa vijana, ili kweli waweze kuwa ni mashuhuda na vyombo vya Uinjilishaji miongoni mwa vijana wa kizazi kipya. Itakumbukwa kwaba, Askofu msaidizi Ruzza alizaliwa kunako mwaka 1963 na kupata Daraja takatifu la Upadre mwaka 1987.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.