2016-06-16 08:47:00

Baraza la Maaskofu Katoliki Austria: familia na wakimbizi!


Kardinali Christoph Schonborn, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Austria ameongoza mkutano wa Baraza la Maaskofu nchini humo kwa siku tatu, ili kujadili pamoja na mambo mengine: wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta hifadhi na usalama wa maisha Barani Ulaya; ndoa na familia, dhana iliyopembuliwa kwa kina na mapana wakati wa maadhimisho ya Sinodi za Maaskofu kuhusu wito na maisha ya ndoa na familia na hatimaye, Baba Mtakatifu Francisko akachapishwa Wosia wa Kitume “Furaha ya upendo ndani ya familia” “Amoris laetitia” ambao Kanisa bado linaendelea kuutafakari, tayari kuumwilisha katika maisha na utume wa Kanisa.

Mkutano huu wa Siku tatu, uliohitimishwa hapo tarehe 15 Juni 2016 umepembua Wosia huu mintarafu hali na mazingira ya Kanisa mahalia nchini Austria kwa kuzingatia mchango uliotolewa na Mababa wa Sinodi za Maaskofu kuhusu familia zilizoadhimishwa kati ya mwaka 2014- 2015. Ni matumaini ya Baraza la Maaskofu Katoliki Austria kwamba, hata vyombo vya habari vilipata tema nyingi zinazoweza kuendelea kufanyiwa kazi kutoka kwenye Wosia wa kitume wa Baba Mtakatifu Francisko “Furaha ya upendo ndani ya familia”.

Maaskofu wametafakari kuhusu wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta hifadhi na usalama wa maisha Barani Ulaya, lakini wanakabiliwa na vikwazo na vizingiti vingi. Maaskofu wamejadili jinsi ambavyo Kanisa linaweza kuwasaidia wakimbizi na wahamiaji, kwa kuwekeza katika mchakato wa maendeleo na ustawi wa jamii; haki na amani, ili kuwasaidia wakimbizi na wahamiaji hawa kupata walau mahitaji yao msingi wakiwa nchini mwao.

Kuna haja ya kusitisha vita na mipasuko ya kijamii ambayo inapelekea makundi makubwa ya watu kuzikimbia nchi zao, amani na utulivu, haki na amani; msamaha na upatanisho vikizingatiwa, kutakuwepo na udhibiti mkubwa wa wimbi la wakimbizi. Kwa wakimbizi waliokwisha kupokelewa kwenye Nchi za Ulaya, basi waingizwe kwenye mchakato wa kuwajumusha katika maisha ya kila siku badala ya mwelekeo wa sasa unaowatenga na kuwanyanyasa wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta usalama na hifadhi ya maisha yao Barani Ulaya.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.