2016-06-14 15:03:00

Njia za kisayansi katika mapambano dhidi ya nyanyaso za kijinsia!


Chuo kikuu cha Kipapa cha Gregorian kilichoko mjini Roma, kwa mara ya kwanza, Jumanne, tarehe 14 Juni 2016 kimetoa diploma kwa wanafunzi waliohitimu masomo yanayolenga kuwalinda watoto wadogo dhidi ya nyanyaso za kijinsia, tukio ambalo limehuhudhuriwa na viongozi wa Kanisa pamoja na wanadiplomasia wanaowakilisha nchi zao nchini Italia. Hii ni sehemu ya mikakati ya Kanisa kama Mama mpendelevu kuendelea kuwalinda watoto wadogo dhidi ya nyanyaso na dhuluma za kijinsia.

Baba Mtakatifu Francisko kwa kutambua na kuheshimu juhudi hizi, ametuma ujumbe wa matashi mema kwa Majaalimu walioendesha kozi hii pamoja na wanafunzi waliofuzu katika masomo haya. Ni matumaini yake kwamba, watasaidia katika sera na mikakati ya Kanisa kuwalinda watoto wadogo pamoja na kuponya donda ndugu la nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo. Mapambano haya anasema Baba Mtakatifu yanahitaji ujasiri na uvumilivu; ukweli na uaminifu; hali itakayosaidia kurejesha tena furaha, amani na utulivu kwa watu wengi.

Kwa upande wake, Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu katika ujumbe wake anasema, ulinzi kwa watoto wadogo dhidi ya nyanyaso za kijinsia ni kipaumbele cha Mama Kanisa katika shughuli na mikakati yake ya kichungaji, ili kupambana na hatimaye, kufutilia mbali vitendo hivi viovu dhidi ya watoto wadogo katika taasisi na vituo vinavyoendeshwa na kumilikiwa na Kanisa Katoliki.

Wanafunzi waliohitimu masomo yao wanatoka katika nchi kumi na tano zilizoko katika mabara manne, ambako udhibiti dhidi ya nyanyaso za kijinsia kwa watoto wadogo, haukuwa umepewa kipaumbele cha pekee. Kumbe, kuna haja ya kuwa na wataalam waliofundwa na kufundika ili waweze kusimama kidete kuzuia na kutibu madonda ya nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo. Makanisa mahalia baada ya kufedheheshwa na nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo yameamua kufanya tafiti na kutoa mafunzo ya kina dhidi ya nyanyaso hizi. Kozi hii itakuwa inatolewa kwa mwaka na kuchukua wanafunzi kati ya 18- 20.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.