2016-06-12 10:01:00

Wagonjwa na walemavu ni sehemu ya Mwili wa Kristo, alama ya upendo!


Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kwa wagonjwa na walemavu imekuwa ni fursa ya kusali, kutafakari na kushirikishana uzoefu na mang’amuzi kuhusu Injili ya maisha na changamoto zake, ili kuliwezesha Kanisa kujenga utamaduni wa ukarimu na huduma ya mapendo kwa wagonjwa na walemavu kwani hawa wanayo siri kubwa inayofichika katika mateso na mahangaiko yao ya ndani. Kilele cha maadhimisho haya ni Ibada ya Misa Takatifu iliyoendeshwa na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican, Jumapili tarehe 12 Juni 2016 kwa ushiriki mkamilifu wa wagonjwa na walemavu katika Liturujia.

Mtakatifu Paulo anasema “Nimesulubiwa pamoja na Kristo; lakini ni hai; wala si mimi tena, bali Kristo yu hai ndani yangu…” maneno ambayo ni muhtasari wa mwelekeo mzima wa Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo kutoka kwa wafu; fumbo ambalo Wakristo wanalishiriki kwa njia ya Ubatizo katika maji na Roho Mtakatifu. Maisha haya mapya yanamwambata mtu mzima: wakati wa magonjwa, mahangaiko hata na kifo, kwani yote haya yamo ndani ya Kristo na yana pata maana kamili kutoka kwake.

Haya yamesemwa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa mahubiri yake kwenye Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kwa wagonwa na walemavu na kwamba, maneno haya yanapata uzito wa pekee kwa wagonjwa na walemavu, hali inayoonesha udhaifu wa mwanadamu pamoja na kujiuliza maswali mazito kuhusu maana ya maisha. Wakati mwingine mwanadamu amekuwa na matumaini makubwa katika maendeleo ya sayansi na tiba ya mwanadamu lakini hata hivyo, bado watu wachache wanapata huduma hii makini na magonjwa bado yana mwandama mwanadamu.

Baba Mtakatifu anasema, haya ni madhara ya dhambi ya asili kiasi kwamba katika utamaduni wa walimwengu mamboleo, mgonjwa na mlemavu ni watu ambao hawana sababu ya kuwa na furaha ya maisha, kwani hawawezi kushiriki kikamilifu katika utamaduni wa raha na machezo; ni katika nyakati kama hizi huduma ya afya inakuwa ni mtaji wa kiuchumi ili kurejesha furaha na utulivu wa ndani mwa wale wanaojiweza kiuchumi, lakini maskini na “akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi” wanakufa katika umaskini wao. Matokeo yake ni kwamba, wagonjwa na walemavu wanatengwa na jamii, ili wasilete usumbufu katika raha za watu.

Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, walimwengu leo hii wanauangalia ugonjwa na ulemavu kwa jicho la kengeza na kwamba, hawataki kujitaabisha kufahamu ukweli wa maana ya maisha ya mwanadamu katika magonjwa na mapungufu yake ya kibinadamu. Walimwengu wanataka kuona ulimwengu wa watu wakamilifu peke yao, wagonjwa na walemavu hawana tena nafasi katika ulimwengu mamboleo. Ikumbukwe kwamba dunia inapata ukamilifu pale ambapo mshikamano wa huruma na mapendo unakua na kushika kasi kati ya watu; kwa kukubaliana na kupokeana jinsi walivyo kwani hata Maandiko Matakatifu yanakaza kusema tena Mungu alivichagua vitu dhaifu vya dunia ili aviabishe vyenye nguvu. Huu ndio mwelekeo wa Injili, Jumapili ya kumi na moja ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa pale Yesu anapomwonesha huruma na mapendo mwanamke mdhambi, aliyehukumiwa na kutengwa na jamii, lakini Yesu anampokea na kumlinda kwa vile amependa sana, upendo ambao ameushuhudia kwa njia ya machozi yake.

Hii ina maanisha kwamba, Mwenyezi Mungu ana upendeleo wa pekee kwa wale wanaoteseka na kumimina machozi kutokana na mahangaiko yao: kiroho na kimwili. Mahangaiko yanayopelekea simanzi katika maisha ya mwanadamu  kwa vile wanakosa upendo; wanatengwa na kusalitiwa na wenzi wao, kiasi kwamba, wanajiona wanyonge wasiokuwa na ulinzi. Hapa kishawishi cha mtu kujifungia katika ubinafsi wake ni kikubwa anasema Baba Mtakatifu Francisko, lakini watu wanapaswa kupenda na kupendwa licha ya mahangaiko yote haya!

Mwanadamu anaweza kufikia furaha ya kweli ikiwa kama ana uwezo wa kupenda na kwamba, hii ni changamoto kubwa katika maisha ya mwanadamu. Wagonjwa na walemavu wanaweza kuandika kurasa mpya za maisha yao pale wanapogundua kwamba, kweli wanapendwa na kuthaminiwa hata katika mambo ya kawaida tu. Kristo Yesu amewapenda watu upeo, kiasi cha kuyamimina maisha yake ili yawe ni fidia kwa wengi wanaoteseka kiroho na kimwili. Hiki ni kielelezo makini cha upendo unaokarimu na kusamahe kwani kwa njia ya mateso yake, wote wameweza kuponywa.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Kristo Yesu ni mganga anayeponya kwa dawa ya upendo kwa kujitwika dhambi na mapungufu ya mwanadamu ili kumkirimia ukombozi, kwani anayafahamu mateso na mahangaiko ya mwanadamu. Yesu ameyaonja kwa njia ya Fumbo la Pasaka. Ulimwengu mamboleo unapaswa kutambua kwamba, ugonjwa na ulemavu ni kielelezo cha upendo unaopaswa kumwilishwa katika uhalisia wa maisha. Waamini wawe na ujasiri wa kukabiliana na mateso pamoja na udhaifu wao wa kimwili kama kielelezo cha uhuru na maana ya maisha, kamwe wasikubali kushindwa na mahangaiko haya, bali wawe tayari kuyaunganisha mateso yao na yale ya Kristo Yesu kwa ajili ya Fumbo la Mwili wake, yaani Kanisa. Huu ni mwili wa Kristo Mfufuka unaotunza bado makovu ya Madonda Matakatifu, kielelezo cha mapambano makali, lakini ni makovu ya madonda yanayoonesha upendo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.