2016-06-08 09:39:00

Mkakati wa maendeleo unalenga kupambana na umaskini Tanzania


Waziri mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amesema Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa wa miaka mitano 2016/2017-2020/2021 unalenga kuboresha maisha ya Watanzania wengi kwa kuhakikisha Sekta zinazoajiri watu wengi na walio masikini zinakuwa kwa kasi. Akizindua Mpango huo Jumanne, Juni 7, 2016 katika ukumbi wa Chuo cha Mipango Mjini Dodoma, Waziri Mkuu Majaliwa amesema Serikali itahakikisha Sekta za Kilimo, Viwanda, Uvuvi na Mifugo zinakua kwa kasi ya kuridhisha ili kuongeza fursa za ajira na kupunguza umasikini. Amesema utekelezaji wa Mpango huo ambao umefungamanisha maendeleo ya viwanda na maendeleo ya watu na unatazamiwa kujibu changamoto ya umasikini Tanzania.

Waziri Mkuu amesema katika Mpango huo kuna maeneo mbalimbali ya vipaumbele yaliyoainishwa katika Mpango huo ni miradi mikubwa kama ya chuma cha Liganga, kufufua shirika la Ndege, Makaa ya Mawe Mchuchuma, ujenzi wa Reli ya Kati kwa kiwango cha standard Gauge ambayo matokeo yake yanatarajiwa kuwa kichocheo cha utekelezaji wa miradi mingine. “Tunatarajia ifikapo mwaka 2025 tuwe tumejenga nchi ambayo ina maisha bora, yenye amani, umoja na utawala bora, jamii inayojifunza na iliyoelimika, yenye uwezo wa kuzalisha na kuwa na ukuaji wa uchumi endelevu na wenye ushindani,” amesema. Waziri Mkuu Majaliwa amesema, azma ya Serikali ni kuhakikisha ukuaji huo wa uchumi unakuwa shirikishi zaidi katika utekelezaji wa Mpango huu na kwamba uendelezaji wa viwanda ndio utakaoleta mafanikio makubwa karika mwelekeo huo.

Katika hatua nyingine Waziri Mkuu Majaliwa amesema jumla ya viwanda 39 kati ya 106 vilivyobinafsishwa kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi ambavyo vilikuwa vya vinazalisha bidhaa za chuma, ngozi, korosho, zana za kilimo, sabuni na mafuta ya kupikia wamevifunga na kushindwa kuviendeleza. Kufuatia hatua hiyo Waziri Mkuu Majaliwa amesema Wizara ya Fedha na Mipango kupitia kwa Msajili wa Hazina itaendelea na zoezi la kuvirejesha viwanda hivyo Serikalini ili waangalie utaratibu mwingine ulio bora wa kuviendeleza kwa kupitia Mpango huo wa Maendeleo. Amesema Mpango huo ambao utajikita zaidi katika kutekeleza mikakati mbalimbali ya kuendeleza viwanda vikubwa, vya kati na vidogo na vile vilivyobinafsishwa ili kuongeza fursa za ajira na kipato kwa wananchi wengi.

Akizungumzia kuhusu utekelezaji wa Mpango wa Kwanza wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano ambao utahitimishwa Juni 30, 2016 Serikali ilifanikiwa kutekeleza miradi ya maendeleo kama ujenzi wa barabara za lami na madaraja ya Kigamboni, Maligisu Nagoo, Mbutu na Ruhekei. Pia ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam (km 542), ujenzi wa mitambo ya kuchakata gesi katika maeneo ya Madimba na Songosongo, ujenzi wa vituo vya kupokelea gesi vya Somanga-Fungu na Kinyerezi.

Na Ofisi ya Waziri mkuu, Dodoma.








All the contents on this site are copyrighted ©.