2016-06-06 10:40:00

Hatima ya amani nchini Burundi iko mikononi mwa wananchi wenyewe!


Rais mstaafu wa Tanzania, Mheshimiwa Benjamin Mkapa, amesema kuwa hatma ya Nchi ya Burundi ipo kwa wana Burundi wenyewe, hivyo amewashauri kukutana makundi yote yanayosigana ili wamalize tofauti zao. Mkapa pia amezitaka nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kuhakikisha nazo zinaendelea kuisaidia nchi ya Burundi ili amani ipatikane. Mkapa ameyasema hayo Jijini hapa wakati  alipokuwa akifungua hivi karibuni kikao cha siku nne cha usuluhishi kwa makundi yanayopingana nchini Burundi kilichokuwa kinafanyika Jijini Arusha, Tanzania.

Amesema wenye jukumu la kuleta amani kwa nchi yao, ni warundi wenyewe na kuwataka kukaa mezani moja ili kujadiliana pamoja na kuondoa tofauti zao kwa manufaa ya nchi yao. Aidha amesema amani ni kitu muhimu kwa mustakabali wa nchi ya Burundi,hivyo ni vyema wakatumia mkutano huo kwaajili ya kumaliza tofauti zao kwa kujadili hoja mbalimbali kwa mustakabali wa nchi yao.

Naye Balozi, Roeland Van der Geer akizungumza kwa niaba ya Jumuiya ya Kimataifa, amesema nchi ya Burundi inatakiwa kuhakikisha, amani inapatikana ili kuhakikisha kila raia wa nchi hiyo anapata maendeleo. Balozi Geer ametoa rai kwa wanaburundi kuhakikisha mgogoro huo wa kisiasa unaisha na nchi inakuwa na amani.

Naye Mjumbe Maalum wa Umoja wa Afrika katika nchi za Maziwa Makuu, Balozi James Benomaar, amesema Jumuiya hiyo inaimani kubwa na Rais Mkapa katika kusuluhisha mgogoro huo na kutoa rai kwa warundi kuhakikisha wanamaliza mgogoro wa nchi yao, ili kupunguza wimbi la wakimbizi wanaokimbilia nchi mbalimbali kwa hifadhi na usalama wa maisha yao. Amesisitiza Warundi wanahaki ya kuishi nchini mwao, hivyo ni lazima tofauti za makundi zikiisha ili kila mtu anufaike na nchi yake hivyo matarajio ya AU ni kuona wananchi wa Burundi wanakaa kwa pamoja, kwa amani na utulivu bila ya kuwa na migogoro ya aina yoyote ile. Hata hivyo Katibu Mkuu wa EAC, Liberat Mfumukeko, Amesisitiza kuwa nchi za EAC, zitashirikiana kwa pamoja katika kutatua mgogoro huo.

Na mwandishi maalum.

 








All the contents on this site are copyrighted ©.