2016-06-03 09:29:00

Uvunjwaji wa haki msingi za binadamu unatishia usalama wa wakimbizi


Askofu mkuu Joseph Buti Thlagale wa Jimbo kuu la Johanesburg, Afrika ya Kusini anasema huduma kwa wakimbizi na wahamiaji Afrika ya Kusini ni sehemu muhimu sana ya maisha na utume wa Kanisa, ili kuhakikisha kwamba, utu, heshima na haki msingi za wahamiaji hawa zinalindwa na kuheshimiwa na wote. Familia ya Mungu nchini Afrika ya Kusini inapaswa kuonesha huruma na ukarimu; kwa kushirikishana habari, sera na mikakati kama sehemu mchakato wa maboresho ya huduma kwa wakimbizi na wahamiaji ambao kwa miaka ya hivi karibuni wamekuwa wakinyanyasika sana nchini Afrika ya Kusini.

Mwakilishi wa Wizara ya Mambo ya ndani kutoka Afrika ya Kusini alibainisha sheria, sera na mikakati inayotekelezwa na Serikali ya Afrika ya Kusini kwa ajili ya wakimbizi na wahamiaji kwanza kabisa ni kuzingatia sheria za kimataifa; kuwarudisha makawao wale wasiokuwa na vibali kisheria na kwamba, Idara ya uhamiaji inaendelea kuboresha huduma kwa ajili ya wahamiaji na wakimbizi nchini Afrika ya Kusini.

Mwakilishi kutoka Shirika ya Wayesuit la Kuwahudumia Wakimbiz, JRS amesema kwamba, kuna wakimbizi wanaotafuta hifadhi ya kisiasa ambao kwa sasa wanakabiliwa na changamoto kubwa katika hupatikanaji wa huduma ya afya kwani hawako kwenye mpango ya hifadhi ya huduma ya afya kijamii. Anasema, wakimbizi na wahamiaji ni watu ambao wanaendelea kuchangia katika mchakato wa ukuaji wa uchumi kitaifa, kumbe si haki kunyimwa huduma ya kiafya.

Sera, sheria na mikakati bora ya huduma kwa wakimbizi na wahamiaji haina budi kuzingatia kwanza kabisa; mafao ya taifa yaani haki msingi na usalama wa raia sanjari na haki msingi za binadamu. Wakati wa utawala wa ubaguzi wa rangi, sheria nyingi zilijikita katika rangi ya mtu na wala si utu na heshima yake kama binadamu. Kunako mwaka 1994 kukafanyika mabadiliko wahamiaji na wakimbizi wakajikuta njia panda: kupokelewa na kukataliwa.

Polisi wakapewa jukumu la kusimamia na kuratibu mchakato wa wahamiaji na wakimbizi Afrika ya Kusini na huo ukawa ni mwanzo wa uvunjaji wa haki msingi za binadamu. Wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji kutoka Zimbabwe lilisababisha mabadiliko makubwa katika sheria na sera za wakimbizi Afrika ya Kusini na kwamba, huduma hii ikahamishiwa kwenye Wizara ya Mambo ya nchi na Waziri mwenye dhamana akapewa mamlaka ya kudhibiti kikamilifu wimbi la wakimbizi, wahamiaji na watu wanaotafuta hifadhi ya kisiasa. Muswada wa Sheria wa Mwaka 2015 kuhusu wakimbizi na wahamiaji ukipitishwa utakuwa na athari kubwa kwa wakimbizi na wahamiaji kutokana na haki msingi za binadamu kutopewa kipaumbele cha pekee katika muswada huu.

Mwakilishi kutoka Msumbiji aliopembua kwa kina na mapana hali ya wakimbizi na wahamiaji kutoka Msumbiji wanaoendelea kutafuta hifadhi na usalama wa maisha kwa nchi jirani. Wakimbizi na wahamiaji hao wanaporejea nchini mwao kutoka Tanzania wanakabiliwa na vikwazo vikubwa. Mwaka 1991 Msumbiji ilitunga sheria ya kudhibiti wimbi la wakimbizi na wahamiaji nchini humo na kwamba, mtu anaweza kupatia uraia wa Msumbiji baada ya kuishi nchini humo kwa zaidi ya miaka kumi. Lakini vita, kinzani na mipasuko ya kijamii nchini Msumbiji inaendelea kusababisha wananchi wengi wa Msumbiji kuikimbia nchi yao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.