2016-06-03 08:23:00

PMS msiogope: Majadiliano, Mageuzi na Upyaisho katika maisha na utume!


Askofu mkuu Protase Rugambwa Katibu Mwambata na Rais wa Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa akizungumza katika mkutano mkuu wa Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa amewashukuru wajumbe wote kwa kushirikisha: Uzoefu na mang’amuzi yao katika mchakato wa Uinjilishaji na Utume wa Kanisa; Sala, Shuhuda na huduma ya upendo kwa Makanisa machanga. Ni matumaini yake kwamba, Kanisa zima litaweza kuwasha moto wa upendo kwa Kristo na Kanisa lake tayari kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo hadi miisho ya dunia.

Itakumbukwa kwamba, mkutano mkuu wa Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa unaowashirikisha pia wakurugenzi wa PMS kitaifa unaongozwa na kauli mbiu “Kuamsha dhamiri ya utume kwa nyakati hizi”. Mashirika haya yapo kwa ajili ya huduma makini kwa Makanisa machanga. Askofu mkuu Rugambwa anakaza kusema, Mashirika haya ya Kipapa yanaweza kuendelea kuwepo ikiwa kama yataendelea kutekeleza dhamana na utume wao kwa ari na moyo mkuu kwa: kuhamasisha, kwa majiundo makini ya awali na endelevu kwa mihimili ya Uinjilishaji kwenye Makanisa machanga zaidi duniani pamoja na kuendelea kushirikiana kwa hali na mali na Makanisa machanga katika maisha na utume wa Kanisa.

Askofu mkuu Rugambwa amesisitiza kwamba, Mashirika haya ya Kipapa si wakala wa kukusanya fedha kwa ajili ya mchakato wa maendeleo endelevu kwa nchi change zaidi duniani, bali ni mashirika ya huduma kwa ajili ya mchakato wa Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili na kwamba, huu ni utambulisho wao kimataifa. Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa ni matunda ya ubunifu wa Mwenyeheri Padre Paolo Manna aliyetaka kuwahamasisha waamini wote kushiriki kwa hali na mali katika mchakato wa Uinjilishaji wa watu. Kumbe, hata leo hii bado kuna haja ya kuamsha dhamiri ya waamini kutambua na kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa.

Wakati huu Kanisa Katoliki linaendelea kufanya mageuzi na upyaisho katika maisha na utume wake. Kumbe, haya Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa hayana budi kushiriki kikamilifu katika mchakato huu, hatua kwa hatua ili kutambua umuhimu wa utume na utambulisho wao ambao kwa miaka mingi umejikita katika huduma ya kifedha kwa ajili ya kuyasaidia Makanisa machanga zaidi duniani. Kwa miaka mingi huduma hii imekuwa na mafao makubwa kwa maisha na utume wa Kanisa, kwa takribani miaka mia moja kwa sasa. Hakuna sababu ya msingi ya kuogopa kufanya majadiliano, mageuzi na upyaisho, ili kuweza kusonga mbele kwa imani na matumaini zaidi.

Katika mkutano huu, Makatibu wakuu wa Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa waliweza kuonesha dira na mwelekeo wa Mashirika haya katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita na hatua ambazo kwa sasa zinachukuliwa kwa ajili ya siku za usoni kama sehemu ya maboresho ya tija na huduma zinazotolewa kwa Makanisa machanga zaidi duniani pamoja na kuendelea kusoma alama za nyakati. Kipindi hiki cha mpito ni fursa ya kujikita katika wongofu wa ndani, ujasiri, ari na moyo mkuu, ili kufanikisha mchakato wa mageuzi ya huduma ndani ya Kanisa, ili kusongesha mbele utangazaji na ushuhuda wa Habari Njema ya Wokovu kwa Watu wa mataifa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.