2016-05-31 08:42:00

Saidieni mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu!


Waamini wanahamasishwa na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba wanampeleka Yesu wa Ekaristi hata pembezoni mwa jamii, ili wote walioko huko waweze kuonja wema, huruma na upendo wake wake unaookoa na kamwe Yesu hataki kubaki akiwa amefungiwa kwenye Tabernakulo. Anataka waja wake wamshuhudie kwa njia ya imani inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican wakati wa kufunga Kongamano la Ekaristi Takatifu Jimbo Katoliki la Cesena nchini Italia, Jumapili tarehe 29 Mei 2016.

Kardinali Parolin ameadhimisha Ibada ya Misa katika Sherehe ya Ekaristi Takatifu kwa mwaliko wa Askofu Douglas Regattieri wa Jimbo Katoliki la Cesena- Sarsina kama sehemu ya mchakato wa kufunga maadhimisho ya Kongamano la saba la Ekaristi Takatifu Kijimbo. Kardinali Parolin pia amewasilisha salam na matashi mema kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko kwa familia ya Mungu Jimboni Cesena ambako pia kuna watawa wa Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu na Masista Waabuduo Damu Azizi ya Yesu kutoka Tanzania wanaofanya utume wao Jimboni humo.

Kardinali Parolin katika mahubiri yake, amekazia umuhimu wa maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu kama chemchemi ya furaha, imani na matumaini kwa waamini kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Waamini wanaposhiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, wanageuzwa na chakula hiki cha Malaika kuwa ni mitume na chachu ya huduma ya huruma na mapendo ndani ya jamii, kielelezo cha imani tendani.

Maadhimisho ya Ekaristi Takatifu katika Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu ni changamoto kwa waamini kuwa na ari na mwamko mpya wa kimissionari, tayari kutoka kimasomaso kumtangaza na kumshuhudia Kristo kwa njia ya matendo ya huruma: kiroho na kimwili; ili kuwaganga na kuwaponya wale waliopondeka moyo; watu wasiokuwa na dira wala mwelekeo sahihi wa maisha, ili wote hawa waweze kuonjeshwa huruma na upendo unaobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake.

Kardinali Parolin anakaza kusema, dhana ya Uinjilishaji mpya inajikita kwa namna ya pekee katika ushuhuda wa maisha wenye mvuto na mashiko; ushuhuda unaobubujika kutokana na mahusiano mema ya waamini na Kristo Yesu kwa njia ya Neno, Sakramenti na huduma ya upendo kwa jirani. Hapa waamini wanahamasishwa na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, wanayafahamu Mafundisho Jamii ya Kanisa, tayari kuyafanyia kazi katika maisha yao ya kila siku. Watambue kwamba, ujasiri, mbinu na hekima vinapata chimbuko lake katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, ili kujenga na kuimarisha jamii.

Kardinali Parolin anaendelea kufafanua kwamba, Ekaristi Takatifu ni chanzo na kiini cha maisha na utume wa Kanisa; Ni sakramenti ya Umoja, Udugu na Mshikamano wa dhati. Hapa waamini wanaalikwa kuwashirikisha jirani zao karama na zawadi ambazo wamekirimiwa na Mungu na hapo wataweza kuona na kushuhudia muujiza wa zawadi na mapaji haya yakiongezeka na kuchanua kwa ajili ya mafao ya wengi, kama alivyofanya Yesu kwa kuwalisha watu wenye njaa kwa mikate mitano na samaki wawili.

Yesu anaweza kuendelea kutenda miujiza lakini anahitaji ushirikiano mkubwa kutoka kwa waja wake na watu wenye mapenzi mema, changamoto na mwaliko wa kuiga mfano wa Wakristo wa Kanisa la mwanzo, kwa kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Waamini wawe na ujasiri wa kumshirikisha Yesu furaha, magumu na matumaini ya maisha yao, ili aweze kuwatia shime, kuwaganga na kuwaponya katika shida na mahangaiko yao. Kardinali Pietro Parolin, akiwa Jimboni Cesena alipata nafasi pia ya kukutana na vijana ambao wanajiandaa kushiriki katika maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2016 Jimbo kuu la Cracovia, Poland. Amewataka vijana hawa kuwa ni wainjilishaji wa vijana wenzao katika ulimwengu mamboleo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.