2016-05-29 10:01:00

Tangazeni na kumshuhudia Kristo kwa njia ya maisha yenye mvuto na mashiko!


Wamissionari wanaotumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa mataifa watambue kwamba, huko ulimwenguni watakumbana na watu waliojifunga katika akili na mawazo yao; upofu wa maisha ya kiroho pamoja na maamuzi mbele kwa wale wasiomfahamu Kristo Yesu, lakini wanajitia ujuzi wa kutaka kumhukumu Mungu. Matokeo na mielekeo kama hii katika maisha ni ukakasi wa moyo au hata pengine nyanyaso na madhulumu dhidi ya mashuhuda na watangazaji wa Habari Njema ya Wokovu.

Lakini ikumbuke kwamba, Yesu Kristo ndiye kiini cha mchakato wa Uinjilishaji anayeliwezesha Kanisa kuzaa matunda kwa wakati wake. Haya yamesemwa na Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu katika Ibada ya Misa Takatifu iliyoadhimishwa hivi karibuni kwenye Kanisa kuu la Bucaramanga, Bogotà, nchini Colombia. Ibada hii ilifunga maadhimisho ya Kongamano la Kimissionari Kitaifa nchini Colombia na ikawa ni fursa kwa Wamissionari wapya kutumwa kwenda sehemu mbali mbali za dunia ili kumtangaza na kumshuhudia Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu!

Kardinali Filoni ambaye amekuwepo nchini Colombia kuanzia tarehe 21- 28 Mei 2016 amewakumbusha wamissionari kwamba, licha ya udhaifu na mapungufu yao ya kibinadamu, hawana sababu msingi ya kushindwa kutoka kifua mbele kumtangaza na kumshuhudia Kristo, hata kama huko njiani watakumbana na vikwazo pamoja na vizingiti vya maisha. Wao wawe imara, daima wakiendelea kukua na kukomaa katika imani, matumaini na mapendo.

Baba Mtakatifu Francisko kutoka Amerika ya Kusini, awe ni chachu ya Uinjilishaji wa kina katika eneo hili, kwani Papa ameleta mwamko mpya wa mahusiano ya watu kwa kushuhudia kuwa ni mchungaji na baba mwema kwa wote. Kwa mfano wa mtindo na maisha yake kama Padre na Askofu, amewagusa watu wengi, kwani kweli amekuwa ni mfano bora wa kuigwa kama mtume na mmissionari, dhana iliyopembuliwa kwa kina na mapana kwenye Mkutano wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Amerika ya Kusini, kule Aparecida.

Ni dhamana ya Wamissionari kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko, kuhakikisha kwamba, wanawaendea na kuwafikia wale wote wanaotamani kuona na kutembea katika mwanga wa Injili unaomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili, ili kweli waamini waweze kuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu kwa waja wake. Kongamano hili la Kimissionari limefanyika wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha Jubilei ya huruma ya Mungu sanjari na Uinjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda wa maisha adili na matakatifu. Kardinali Filoni, analitaka Kanisa nchini Colombia kuwa ni sehemu ya mchakato wa huduma ya upendo kwa maskini na wale wote wanaosukimizwa pembezoni mwa jamii, ili wote waweze kukutana na Kristo Yesu katika hija ya maisha yao kwa njia ya Wamissionari wa Injili ya furaha!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.