2016-05-29 07:41:00

Ekaristi Takatifu ni chemchemi ya utume wa Kanisa!


Maadhimisho ya Sherehe ya Ekaristi Takatifu nchini Italia imekuwa pia ni fursa kwa waamini kuanza maandalizi ya maadhimisho ya Kongamano la 26 la Ekaristi Takatifu kitaifa, kuanzi tarehe 15 – 18 Septemba 2016. Tukio hili litawashirikisha Maaskofu na wajumbe kutoka katika kila Jimbo, ili kujenga na kuimarisha madaraja ya waamini kukutana na kusali, lakini zaidi ni tukio la kuimarisha imani ya Kanisa katika Fumbo la Ekaristi Takatifu, chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa.

Maadhimisho haya kwa mwaka huu yatafanyika Jimbo kuu la Genova, ambako waamini wataweza kuadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu, Kuabudu Ekaristi Takatifu na hatimaye kushuhudia imani yao kwa Fumbo la Ekaristi Takatifu wakati wa maandamano kuzunguka viunga na mitaa ya mji wa Genova. Kardinali Angelo Bagnasco, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia katika barua yake ya mwaliko kwa maadhimisho haya anakaza kusema, Kongamano la Ekaristi Takatifu Kitaifa na Kimataifa ni sehemu ya Utamaduni na Mapokeo ya Kanisa kama sehemu ya ushuhuda wa Injili ya furaha na imani kwa Kristo Yesu anayeendelea kubaki kati ya waja wake kwa njia ya Fumbo la Ekaristi takatifu.

Waamini wanahamasishwa kujiandaa kikamilifu ili hatimaye, kuweza kuadhimisha Fumbo hili la imani linalopaswa kumwilishwa katika familia na Jumuiya za Kikristo kwa kuhakikisha kwamba, kunakuwepo na ushiriki mkamilifu katika Ibada ya Misa takatifu na tafakari ya Neno la Mungu linalomwilishwa katika ushuhuda wa matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu ni fursa ya kukutana na Kristo katika Neno la Meza ya huruma, upendo na huduma.

Waamini wanaposhiriki katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu wamwachie nafasi Kristo ili aweze kuwamegea huruma na upendo wake kwa njia ya Neno na hatimaye, wokovu unaobubujika kutoka katika Fumbo la Msalaba. Fumbo la Ekaristi Takatifu ni ushuhuda wa uwepo endelevu wa Yesu Kristo Mkombozi wa ulimwengu anayetembea na waja wake hadi utimilifu wa dahali. Uwepo wake unafichika katika maumbo ya Mkate na Divai; Sakramenti ya Upendo na chakula safi cha wasafiri kuelekea mbinguni kwa Baba.

Ekaristi Takatifu ni chachu ya huruma na upendo wa Mungu kwa mwanadamu. Uwepo wa Yesu katika Tabernakulo ni kielelezo cha mwanga angavu na uwepo wa Mungu kati ya watu wake. Kardinali Bagnasco anakumbusha kwamba, Kanisa ni Fumbo la Mwili wa Kristo linaloendelea kuboreshwa kwa njia ya: unyenyekevu wa moyo, sala na upendo uliopyaishwa na kufumbatwa kwenye Jumuiya za Kikristo zilizotakaswa kwa Damu Azizi ya Kristo.

Maadhimisho ya Kongamano la XXVI la Ekaristi Takatifu Kitaifa nchini Italia yanaongozwa na kauli mbiu “Ekaristi ni chemchemi ya utume”. Hii inatokana na ukweli kwamba, Kanisa linalojikita katika Ekaristi, hili ni Kanisa la kimissionari linalotumwa kutangaza na kushuhudia huruma na upendo wa Mungu katika maisha ya watu! Waamini wanahamasishwa kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya upendo unaobubujika kutoka katika Sakramenti ya Ekaristi Takatifu kwa kushuhudia kile walichoona na kusikia, kwa kuwatangazia wengine, ili wao pia waweze kushiriki na hatimaye, kufumbatwa katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Kardinali Angelo Bagnasco anahitimisha barua ya mwaliko kwa familia ya Mungu nchini Italia kujiandaa vyema kwa ajili ya maadhimisho ya Kongamano la Ekaristi Takatifu kitaifa, ili hatimaye, kuvuna matunda yanayokusudiwa yaani: toba, wongofu wa ndani na utakatifu wa maisha!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.