2016-05-28 14:54:00

Papa akutana na watoto waliotikiswa kwa kifo!


Umati wa watoto uliokuwa umepanda “Treni ya watoto” kutoka Calabria, Kusini mwa Italia, uliwasili kwa shangwe na bashasha mjini Vatican na kukutana na Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi, tarehe 28 Mei 2016. Hili ni tukio la kila mwaka ambalo huandaliwa na Baraza la Kipapa la Utamaduni, ili kuwapatia watoto nafasi ya kukutana na kuzungumza na Khalifa wa Mtakatifu Petro pamoja na kuendeleza majadiliano na waamini wa dini mbali mbali. Baadhi ya watoto hawa wamemwomba Baba Mtakatifu kuwakumbuka na kuwaombea ndugu na jamaa zao ambao wametangulia mbele ya haki.

Treni hii maalum ilibeba watoto ambao hata kabla ya kuanza kusherehea Injili ya uhai wameonja mateso na magumu ya maisha, kiasi hata cha kuchungulia kifo. Wengi wa watoto hawa ni wale wanaohudumiwa na Jumuiaya ya Mtakatifu Yohane wa XXIII. Ni watoto kutoka katika mataifa mbali mbali. Baadhi ya watoto kutoka Calabria wamechanga fedha kidogo na kumkabidhi Baba Mtakatifu Francisko kama mchango wao na kwamba, wanaahidi kuwaonjesha watoto wenzao huruma na upendo bila kujali rangi ya ngozi yao, dini au mahali wanapotoka.

Baba Mtakatifu amesikiliza ndoto za watoto hawa kwa umakini mkubwa; Ukumbi wa Paulo VI ukageuka kuwa ni ukumbi wa majibu na maswali; kicheko na furaha. Baba Mtakatifu Francisko amewaonesha watoto hao picha ya mawimbi ya bahari na jua; haya ni mawimbi ambayo yanaendelea kusababisha vifo vya wahamiaji na wakimbizi wengi huko kwenye Bahari ya Mediterrania. Baba Mtakatifu amewaonesha watoto hao zawadi ya mavazi ya kuokolea aliyopewa na kundi la waokoaji waliomweleza kwamba kuna mtoto aliyefari dunia kwa kuzama bahari na wao walishindwa kuokoa maisha yake na badala yake wakabaki na vazi la kuokolea maisha.

Baba Mtakatifu amewaambia watoto hawa kwamba, kuna makundi makubwa ya watu ambao yako hatarini. Watoto wengi wanakufa maji na ambao kamwe majina yao hayatafahamika, lakini wao kwa sasa wako mbinguni. Kuna watu wanaotafuta usalama na hifadhi ya maisha, lakini wanakumbukana na pazia la chuma. Mtu ambaye anashindwa kuguswa na mahangaiko ya jirani zake, hana kabisa moyo wa ubinadamu.

Baba Mtakatifu amewaambia watoto hawa kwamba, Yesu anakazia kwa namna ya pekee: upendo, amani, umoja, udugu na mshikamano; usawa, mafao ya wengi na huruma pasi na mipaka. Watoto wamemuulizia Baba Mtakatifu maana ya Upapa katika maisha yake na kuwajibu kwamba, ni kutenda mema kadiri ya uwezo wake. Kila mtu anapaswa kutenda kadiri ya wito na dhamana yake ndani ya Kanisa na katika jamii husika. Kwa hakika, watoto wamefurahia kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu, tukio ambalo pengine litakuwa ni vigumu kuweza kufutika machoni na mioyoni mwao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.