2016-05-28 11:32:00

Mh. Padre Paul Horan, ateuliwa kuwa Askofu mpya wa Jimbo la Mutare!


Baba Mtakatifu Francisko ameridhia ombi la kung’atuka kutoka madarakani lililowasilishwa kwake na Askofu Alexio Churu Muchabaiwa wa Jimbo Katoliki Mutare, Zimbabwe kadiri ya Sheria za Kanisa namba 401§ 1. Wakati huo huo, Baba Mtakatifu amemteua Mheshimiwa Padre Paul Horan, O. Carm kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki Mutare, Zimbabwe.

Askofu mteule Paul Horan alizaliwa tarehe 17 Oktoba 1962 huko Ireland. Baada ya kukamilisha majiundo yake ya kitawa, kunako tarehe 15 Oktoba 1995 akaweka nadhiri zake za daima na hatimaye kupewa Daraja Takatifu la Upadre tarehe 17 Juni 1997, huko Ireland. Kabla ya kujiunga na maisha ya kitawa, aliwahi kuwa ni mfanyakazi katika Kampuni ya wahasibu nchini Ireland. Kunako mwaka 2001 akajiendeleza katika masomo ya taalimungu na kujipatia Shahada ya uzamili kutoka “Catholic University of America” kilichoko huko Washington, DC. Marekani. Akawasili nchini Zimbabwe kama mmissionari kunako mwaka 2001.

Katika maisha yake kama Padre alitumia kipindi cha mwaka mmoja yaani mwaka 2001 kujifunza lugha, mila na tamaduni za Kishona, huko Zimbabwe. Mwaka 2001- 2004 alikuwa Padre mlezi wa watakaji. Mwaka 2004- 2006 akateuliwa kuwa Mkurugenzi wa Wanovisi wa Mapadre Wakarmelitani. Mwaka 2006 – 2008 akateuliwa kuwa Wakili Paroko, Parokia ya St. Kilian, huko Makoni, Jimbo Katoliki la Mutare. Mwaka 2008 akateuliwa kuwa Mkurugenzi wa Shule Katoliki ya Kriste Mambo, huko Rusape, huduma ambayo ameiendeleza hadi kuteuliwa kwake kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki Mutare, Zimbabwe.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.