2016-05-28 11:58:00

Majadiliano ya kidini na kitamaduni; haki msingi za binadamu ni muhimu!


Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 28 Mei 2016 amekutana na kuzungumza na Rais Tony Tan Keng Yam wa Jamhuri ya Singapore na baadaye amepata pia nafasi ya kukutana na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican aliyekuwa ameambatana na Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican.

Katika mazungumzo, viongozi hawa wawili wamegusia mahusiano mazuri yaliyopo kati ya Vatican na Jamhuri ya Singapore; ushirikiano mwema kati ya Kanisa na Serikali hususan katika medani za elimu na maendeleo jamii. Baadaye, Baba Mtakatifu pamoja na mgeni wake, wamegusia mada zinazojiri katika masuala ya kimataifa na hali ya kisiasa kikanda. Kwa namna ya pekee, wamekazia umuhimu wa kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini na kitamaduni sanjari na kuendeleza mchakato wa kulinda haki msingi za binadamu, utulivu, haki na amani huko Kusini Mashariki wa Bara la Asia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.  








All the contents on this site are copyrighted ©.