2016-05-28 07:12:00

Jengeni utamaduni wa majadiliano ili kudumisha amani Kenya!


Viongozi wa kidini nchini Kenya katika ujumbe wao kwa familia ya Mungu nchini humo wakati huu wa mchakato kuelekea uchaguzi mkuu nchini Kenya unaotarajiwa kufanyika mwaka 2017, wanawataka Wakenya wote kuonesha uzalendo na hatimaye, kujenga utamaduni wa kujadiliana na kusikilizana, ili kudumisha amani, ustawi na maendeleo ya wengi. Kinzani kuhusu Tume huru ya uchaguzi nchini Kenya na Tume ya mipaka ni mambo yanayohatarisha amani, umoja na mshikamano wa kitaifa kwa wakati huu.

Viongozi wa kidini katika tamko lao wanatoa salam za rambi rambi kwa wote waliofikwa na mkasa wa kuondokewa na ndugu, jamaa na rafiki zao wakati wa maandamano yaliyofanyika hivi karibuni nchini Kenya na kusababisha maafa na uharibifu mkubwa wa mali za watu. Viongozi wa kidini wanawataka wananchi wa Kenya kujenga na kudumisha utamaduni wa majadiliano unaojikita katika haki msingi za binadamu, usawa, uhuru, demokrasia, haki jamii na utawala wa sheria mambo msingi yanayopewa kipaumbele cha pekee katika Katiba ya Kenya.

Viongozi wa kidini wanawataka wanasiasa na wapambe wao kuzingatia mafao ya wengi pamoja na serikali kuwahusisha wapinzani katika matukio ya kitaifa. Wanaonya kuwa wanasiasa watawajibika mbele ya wananchi wa Kenya, ikiwa kama watalitumbukiza taifa katika maaafa kama ilivyojitokeza kwenye uchaguzi mkuu uliopita. Ili kufikia muafaka wa kweli familia ya Mungu nchini Kenya haina budi kujikita katika majadiliano yanayojikita katika ukweli, uwazi na urafiki.

Mwishoni, viongozi wa kidini nchini Kenya katika tamko lao kwa vyombo vya habari wanalitaka Bunge, kukamilisha masuala yote yanayohusiana na mchakato wa uchaguzi, ili kujenga mazingira bora zaidi kwa ajili ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika kunako mwaka 2017. Wananchi wa Kenya wanahamasishwa kuzingatia: amani na umoja wa kitaifa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.