2016-05-27 14:15:00

Mashemasi ni wahudumu wa Injili ya huruma na mapendo!


Mashemasi wa mpito na mashemasi wa kudumu kutoka sehemu mbali mbali za dunia, kwa sasa wako mjini Roma ili kuadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kwa Mashemasi. Jumapili, tarehe 29 Mei 2016, saa 4:30 kwa saa za Ulaya, Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kuhitimisha maadhimisho ya Jubilei ya Mashemasi.

Itakumbukwa kwamba, kuna makundi mawili ya Mashemasi ndani ya Kanisa. Kuna Mashemasi wa mpito kuelekea Daraja Takatifu la Upadre na kuna Mashemasi wa kudumu ambao wengi wao ni watu wa familia, lakini wanajisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma ya Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa kadiri ya Sheria za Kanisa, lakini zaidi huduma ya upendo inayomwilishwa katika matendo ya huruma kiroho na kimwili.

Huduma ya Sakramenti ya Daraja Takatifu tangu mwanzo, imegawanyika katika sehemu kuu tatu: Uaskofu ambao ni utimilifu wa Sakramenti ya Daraja; Upadre na Ushemasi. Kumbe, Mashemasi ni wasaidizi wakuu wa Maaskofu na Mapadre. Mashemasi hushiriki kwa namna ya pekee utume na neema ya Kristo kwa kupewa chapa isiyofutika na hufananishwa na Kristo aliyejifanya “Shemasi” yaani mtumishi wa wote.

Mashemasi ni wahudumu wakuu wakati wa maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa, hasa wakati wa Ibada ya Misa Takatifu. Mashemasi wanaweza kusimamia na kubariki Ndoa Takatifu. Ni wahudumu wa Neno kwa kutangaza, kuhubiri na kulishuhudia katika huduma mbali mbali za upendo. Dhana ya Mashemasi wa kudumu, ambao kimsingi wanapewa Ushemasi wa huduma kadiri ya mafundisho ya Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, Barani Afrika ni wachache sana, lakini kazi ya huduma kwa kiasi kikubwa inatekelezwa na Makatekista.

Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI katika Waraka wake wa kitume, Dhamana ya Afrika, “Africae munus” ameweka mkazo juu ya umuhimu wa Mashemasi wa kudumu kama sehemu ya kuendeleza mchakato wa kimissionari. Mashemasi wa kudumu wanapaswa kujivunia kazi yao njema wanayoitekeleza kwa nguvu ya kimaadili kwa kuheshimu tunu ya uaminifu, ukweli, furaha na mafao ya wengi. Mashemasi katika ujumla wao wanahimizwa kutoa huduma ya pekee kwa wagonjwa wa kiakili na kimwili; maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii na kwamba, upendo na huruma ya Kristo iwafikie na kuwaambata wote!

Kwa nama ya pekee, Mashemasi wanapoadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, Maaskofu wanahimizwa kuwapatia majiundo makini mashemasi wao, ili wawe kweli ni mfano bora wa kuigwa kama ilivyokuwa kwa Mashemasi watakatifu Stefano, Mtakatifu Laurenti, Mtakatifu Vincenti pamoja na mashemasi wengi ambao wamekuwa ni mashuhuda wa imani, matumani na mapendo. Daima watafute kumtambua na kukutana na Kristo katika Fumbo la Ekaristi Takatifu na katika huduma makini kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Huduma ya Altare na upendo kwa maskini iwe ni chachu ya utakatifu wa maisha. Mashemasi kwa hakika ni wahudumu wa Injili ya huruma na mapendo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.