2016-05-25 07:33:00

Injili ya familia ni furaha ya ulimwengu!


Injili ya familia ni furaha ya ulimwengu ndiyo kauli mbiu ya maadhimisho ya Siku ya tisa ya Familia Kimataifa, itakayoadhimishwa kuanzia tarehe 22- 26 Agosti, 2018 Jimbo kuu la Dublin, nchini Ireland. Uzinduzi wa mchakato wa maadhimisho haya umefanyika mjini Vatican, Jumanne, tarehe 24 Mei 2016 na Askofu mkuu Vincenzo Paglia, Rais wa Baraza la Kipapa la Familia na kuhudhuriwa na Askofu mkuu Diarmuis Martin wa Jimbo kuu la Dublin, Ireland.

Askofu mkuu Paglia akizungumza na waandishi wa habari amesema kwamba, hili litakuwa ni tukio la kwanza kimataifa kuadhimishwa na Mama Kanisa, baada ya maadhimisho ya Sinodi za Maaskofu na hatimaye, kuchapishwa kwa Wosia wa kitume wa Baba Mtakatifu Francisko “Furaha ya Upendo ndani ya familia” “Amoris laetitia” ambao kwa sasa ni mwongozo wa maisha na utume wa familia ndani ya Kanisa Katoliki.

Wosia huu ni changamoto kubwa kwa Makanisa mahalia kuhakikisha kwamba, yanapyaisha maisha na utume wa familia, ili kuwa na mwelekeo mpya unaojikita katika toba, wongofu wa ndani na utakatifu wa maisha unaombata huruma ya Mungu. Mama Kanisa anawahamasisha watoto wake kuhakikisha kwamba, wanatoa kipaumbele cha kwanza kwa tunu msingi za maisha ya ndoa na familia yanayowawezesha kutangaza na kushuhudia Injili ya familia, kielelezo cha imani tendaji.

Maadhimisho ya Siku ya Familia Kimataifa yanafanyika kwa mara nyingine tena anasema Askofu mkuu Paglia Barani Ulaya, mahali ambako kwa sasa kuna changamoto nyingi kuhusu maisha na utume wa familia. Itakumbukwa kwamba, maadhimisho ya Siku ya Nane ya Familia Kimataifa mwaka 2015 yaliadhimishwa Jimbo kuu la Philadelphia, nchini Marekani na kuhudhuriwa na Baba Mtakatifu Francisko. Ireland kwa sasa inapitia kipindi kigumu cha historia na maisha yake. Maadhimisho haya yanalenga pia kuitia shime familia ya Mungu nchini Ireland kusonga mbele kwa imani na matumaini pasi na kukata tamaa, kwa kuambata changamoto za kimissionari, tayari kutangaza na kushuhudia tunu msingi za maisha ya ndoa na familia. Ni fursa ya kutambua na kuendeleza wito na utume wa ndoa na familia ndani ya Kanisa na Jamii katika ujumla wake.

Ni matumaini ya Baraza la Kipapa la familia kwamba, waamini wa dini mbali mbali, wanasiasa na watunga sera wataweza kuchangia kwa kina na mapana katika kupambana na changamoto zinazokabili maisha na utume wa familia, ili kuondokana na ubinafsi pamoja na mtazamo hasi kuhusu tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, ili kweli maisha ya kiroho yaweze kupata nafasi katika ustawi na maendeleo ya familia ya binadamu!

Kwa upande wake, Askofu mkuu Martin anasema, maadhimisho ya Siku ya tisa ya familia kimataifa huko Ireland ni sehemu ya mchakato wa upyaisho wa maisha na utume wa Kanisa, changamoto inayovaliwa njuga kwa sasa na Baba Mtakatifu Francisko kwa wakati huu, sanjari na kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maisha na utume wa familia, shule ya haki, amani, upendo, utakatifu, imani na matumaini. Kumbe, maadhimisho haya ni mwendelezo wa mchakato wa upyaisho na mageuzi ndani ya Kanisa kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maisha na utume wa familia.

Hii ni changamoto na mwaliko wa kuambata huruma na upendo wa Mungu, hasa wakati huu wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, familia ziwe kweli ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu! Maadhimisho haya itakuwa ni fursa ya kimwilisha matunda ya maadhimisho ya Sinodi za Maaskofu na utimilifu wake ni wosia wa kitume “Furaha ya upendo ndani ya familia”. Mkazo ni kuendeleza katekesi ya maisha ya ndoa na familia ili kupambana na changamoto dhidi ya tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, ili kweli waamini waweze kuwa ni mashuhuda na vyombo vya Injili ya familia inayobubujika kutoka katika undani wa maisha ya familia!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican








All the contents on this site are copyrighted ©.