2016-05-24 07:08:00

Familia ni wakala wa haki, amani, upendo na maridhiano katika jamii!


Familia ya Mungu Barani Afrika katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Huruma ya Mungu inaalikwa kwa namna ya pekee kabisa kuwa kweli ni mashuhuda wa Injili ya huruma na familia kwa kutambua kwamba, familia ni wakala wa huruma na amani katika jamii. Hii ndiyo changamoto ambayo imefanyiwa kazi hivi karibuni na Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria, tukio ambalo liliandaliwa na Idara ya Familia, Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria.

Katika mahubiri yake, Askofu mkuu Augustine Akubeze, Makamu wa Rais, Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria alikaza kusema, familia ni chachu ya mafanikio ya taifa lolote lile, kumbe, hapa kuna haja ya kutambua na kuthamini mchango mkubwa unaotolewa na familia katika maisha na utume wa Kanisa na Jamii katika ujumla wake.

Taifa ambalo linasimikwa katika familia madhubuti, lina uwezekano wa kucharuka katika sera na mikakati ya maendeleo endelevu! Familia goi goi na chovu ni kikwazo kikubwa cha ustawi na maendeleo ya wengi! Kama kweli familia ya Mungu Barani Afrika inataka kucharuka katika sera na mikakati ya maendeleo endelevu inayotekelezeka, kuna haja ya kuziwezesha familia ili kweli ziweze kutekeleza dhamana na wajibu wake katika jamii, kwani familia ni kitovu, msingi na mahali ambapo watu wanafundishwa kwa mara ya kwanza kanuni maadili, utu wema, imani, ukweli, upendo, msamaha, umuhimu wa kazi na matumaini kwa Mwenyezi Mungu

Askofu mkuu Akubeze, anasema kuna haja kwa wazazi kuhakikisha kwamba, wanatekeleza dhamana na wajibu wao katika kurithisha imani, kuonya na kuwaongoza vyema watoto wao katika maadili na utu wema. Wazazi na walezi kamwe wasikate tamaa katika utume na malezi kwa watoto wao na kwamba, mapambano ya kweli dhidi ya rushwa na ufisadi yanaanza ndani kabisa ya familia kwa njia ya ushuhuda na mfano bora wa kuigwa unaotolewa na wazazi wenyewe!

Inasikitisha kuona kwamba, kuna baadhi ya wazazi na walezi wanakuwa mstari wa mbele katika wizi wa mitihani na rushwa katika nyanja mbali mbali, hali ambayo inawajengea watoto usugu katika kushindwa kuishi kanuni maadili na utu wema. Familia ya Mungu nchini Nigeria inahamasishwa kwa namna ya pekee kabisa kuendelea kufanya tafakati ya kina kuhusu Wosia wa Kitume uliotolewa na Baba Mtakatifu Francisko Furaha ya Upendo ndani ya familia, “Amoris laetitia” ili kuweza kusimama imara na thabiti katika kutangaza na kushuhudia Injili ya Familia inayojikita katika chemchemi ya maisha, huruma na mapendo kutoka kwa Kristo na Kanisa lake!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican








All the contents on this site are copyrighted ©.