2016-05-04 07:25:00

SACBC: Huduma ya afya ipewe kipaumbele cha kwanza na wala si silaha!


Umaskini wa hali na kipato, ukosefu wa fursa za ajira pengo kubwa kati ya matajiri na akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi ni kati ya mambo makubwa yanayohatarisha ulinzi, usalama, umoja na mshikamano wa kitaifa nchini Afrika ya Kusini. Matokeo yake mchakato wa ujenzi wa misingi ya haki, amani na upatanisho unaendelea kufifia siku hadi siku na badala yake, mmong’onyoko wa kanuni maadili na utu wema unaendelea kushika kasi ya ajabu miongoni mwa wananchi wa Afrika ya Kusini.

Haya ni kati ya mambo makuu yanayozungumziwa na Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Kusini mwa Afrika kutokana na changamoto kadhaa za kisiasa zilizojitokeza nchini humo hivi karibuni baada, Mahakama kuu nchini Afrika ya Kusini kumkuta hana hatia ya rushwa na ufisadi wa mali ya umma. Kunako mwaka 1999 Serikali ya Afrika ya Kusini ilinunua kiasi kikubwa cha silaha, manunuzi ambayo hayakuzingatia sheria na kanuni za nchi.

Askofu Abel Gabuza, Mwenyekiti wa Tume ya haki na amani ya Shirikisho la Mabaraza la Maaskofu Kusini mwa Afrika, SACBC anasema, kulikuwa hakuna haja kwa Serikali ya Afrika ya Kusini kununua kiasi chote hiki cha silaha na badala yake, fedha hii ingeweza kutumika kwa ajili ya kununulia dawa na vifaa tiba ili kuboresha sekta ya afya nchini humo, ambayo kwa sasa inakabiliwa na changamoto nyingi!

Maaskofu wanakaza kusema, hata kama hakuna harufu ya rushwa na ufisadi katika manunuzi ya silaha nyingi kiasi hiki, lakini hiki ni kielelezo cha ukiukwaji mkubwa wa kanuni maadili, kwani wakati ule, Serikali ilikuwa inashindwa kununua dawa kwa ajili ya wananchi wake, lakini ikawa na ujasiri wa kununua silaha nyingi kiasi kile! Hadi sasa hakuna tishio la Afrika ya Kusini kuvamiwa kutoka nje, kumbe hakuna sababu ya msingi ya kununua na kulimbikiza silaha, wakati ambapo kuna umaskini mkubwa na ukosefu wa fursa za ajira unaowaandama wananchi wengi wa Afrika ya Kusini.

Maaskofu wanafafanua kwamba, tishio kubwa la amani, usalama na umoja wa kitaifa ni tatizo la ukosefu wa fursa za ajira miongoni mwa vijana; mipasuko ya kijamii inayotokana uwepo wa pengo kubwa kati ya matajiri na maskini; hali ambayo inachangia kwa kiasi kikubwa maandamano, migomo na mitafaruku ya kijamii ambayo kwa siku za hivi karibuni, imekuwa kana kwamba ni sehemu ya maisha ya wananchi wa Afrika ya Kusini. Maaskofu wanaiomba Serikali ya Afrika ya Kusini kusitisha mkabata wa kutaka kununua vinu vya kutengeneza nishati ya nyuklia nchini Afrika ya Kusini.

Maaskofu wanasema, umefika wakati kwa familia ya Mungu nchini Afrika ya Kusini kusimama kidete kupambana kufa na kupona na saratani ya rushwa na ufisadi wa mali ya umma; ili kujenga umoja na mshikamano wa kitaifa pamoja na kung’oa kabisa ubaguzi wa rangi ambao bado unaendelea kuwatesa wananchi wa Afrika ya Kusini. Afrika ya Kusini, iwajali na kuwasaidia wananchi wake wanaoogelea katika dimbwi la umaskini wa hali na kipato, sanjari na kuboresha hali ya maisha ya wananchi wengi ambao hawajaridhika na sera na mikakati ya uchumi na maendeleo Afrika ya Kusini. Serikali ijikite zaidi katika ulinzi na usalama wa maisha na mali ya wananchi wake, ili kweli sera za afya na uchumi ziwalenge maskini zaidi nchini Afrika ya Kusini!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.