2016-05-04 14:36:00

Papa sema kila mtu amealikwa kuifurahia huruma ya Mungu


Katekesi ya Baba Mtakatifu Francisko kwa Jumatano hii, inasema, watu wote wamealikwa kuifurahia huruma ya Mungu, yenye kumjali kila mmoja, kama inavyotajwa katika mfano wa Mchungaji mwema, kwenye Injili. Papa Francisko alieleza  kama sehemu ya mwendelezo wa katekesi zake juu ya huruma, anazotoa kwa wakati huu wa Jubilee maalum ya mwaka Mtakatifu wa  Huruma.  Ameitafakari huruma ya Mungu kwa kurejea  mfano wa  Mchungaji Mwema, aliyeacha kundi la wanakondoo  na kwenda kumtafuta mmoja aliyekuwa amepotea akisema,  inaonyesha upendo na ukaribu wa Mungu kwa wenye dhambi.

Papa aliendelea kusema mfano huu unalenga  kuelewesha zaidi juu ya  ukaribu wa Yesu kwa wenye dhambi, ili kutenda dhambi isiwe kashfa isiyosamehewa,  lakini iwe kinyume chake, imwezeshe  mtu kutafakari jinsi anavyoiishi imani yake. Anasema kwa upande mmoja tunaona wenye dhambi wanaojongea karibu Yesu na kumsikiliza na kwa upande mwingine tunawaona walimu wa Sheria, Mafarisayo na waandishi wakituhumu  kwamba ni  kinyume cha sheria kukaa na wadhambi. Na wanamshutumu Yesu kwa kujichanganya na  wenye dhambi.  Majadiliano ya walimu na Mafarisayo na waandishi,   yanayonyesha  ukaidi  na majivuno , wakidhani  ni wao peke yao wenye haki.

Kwa hiyo katika mfano huu , Papa aliongeza,  tunaona sifa za watu watatu , Mchungaji , Kondoo mpotevu na kundi kubwa la kondoo.  Papa amesema, Yesu aliutumia mfano huu , kutuonyesha ukaribu wake kwa wakosefu ili wakosefu wasionekane kama ni kashfa isiyosamehewa. Lakini kumbe kinyume chake, kosa la mwingine la limhimize kila mmoja kutafakari kwa makini, hali yake ya kiroho na   kwa namna gani anaiishi imani yake. Mfano huu unaonyesha  kwa upande mmoja jinsi mwenye dhambi anavyogusa moyo wa Yesu, anayetoka na kwenda kumtafuta na kumsikiliza na kwa upande mwingine tunaona walimu wa sheria na mafarisayo, wasivyotambua kwamba huruma ya Mungu ni kwa watu wote hata wadhambi.  

Katika mfano huu pia,  binadamu wanaonyeshwa kwamba,  Mungu hataki hata mtu mmoja apotee. Kwa  huruma yake isiyokuwa na mwisho wala kipimo,  inaonyesha yuko tayari kukutana na binadamu wote mahali popote na katika hali zote.

Hivyo Katika katekesi hii, Papa Francisko, ametoa himizo la kutafakari mfano huu katika ngazi za kijumuiya  za Kanisa , kuhakikisha kwamba hakuna anayepotelea mbali bila kutafutwa. Ni lazima kuwatafuta wale wanaotaka kujitenga mbali na jumuiya, kwa sababu mbalimbali zenye kuwakatisha tamaa.  Mfano huu wa  Mchungaji Mwema, na iwe kichocheo na changamoto ya kutoka nje na kwenda kuwatafuta hasa waliopotoka. Pia Yesu anafundisha kuwa  macho daima ili asiwepo mwanakondoo anayepotea, na kama watatokea kuwapo ni lazima kwenda kuwatafuta na kuwarudisha kundini.

Papa anawataka Wakristo wote kijifunga kibwebwe na kutoa nje kwenda kuuihubiri Injili ya upendo wa kuokoa, na siwepo Mkristo anayebaki amefungia imani moyoni mwake tu bila kuitoa nje kwa wenigine,  au kujifungia kama jumuiya ndogo au kama  parokia, , lakini wote na watoke nje kwa lengo la kukutana na wengine na kuwashuhudia huruma ya Mungu kwamba ni kwa watu wote.  Hiyo ndiyo iwe furaha ya moyo mchungaji mwema, na furaha ya muumini Mkristo na Kanisa lote,ili  kwamba hakuna anayepotelea mbali, kwa kuwa sisi sote, tulikuwa wanakondoo waliopotea,  tuliokombolewa na Huruma ya Bwana. Kumbe sisi sote, tumeitwa kufurahi katika upendo wake wenye huruma, na kuupeleka  upendo  na huruma hiyo kwa  wengine, na hatimae kuuungana pamoja kama wanakondoo wa zizi moja waliookolewa  kwa huruma ya Mungu .  








All the contents on this site are copyrighted ©.