2016-05-03 08:14:00

Omba omba wa Bara la Ulaya kukutana na Papa Francisko, Novemba 2016


Ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia unaendelea kushuhudia wimbi kubwa la maskini na watu wanaoishi katika mazingira hatarishi kila kukicha. Haya ni matokeo ya mifumo ya uchumi na utandawazi usiojali mateso na mahangaiko ya watu; mipasuko ya kijamii, vita, kinzani, majanga na maafa asilia. Kuna wimbi kubwa la maskini linaloendelea kujitokeza Barani Ulaya kutokana na ukosefu wa fursa za ajira na mipasuko ya kijamii na kisiasa, kiasi kwamba, wanajikuta wengi wao wakiishia katika umaskini mkubwa wa hali na kipato!

Baba Mtakatifu Francisko anasema, maskini ni kiini cha Habari Njema ya Wokovu, wanapaswa kuheshimiwa, kupendwa na kusaidiwa kwani wao pia wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kuanzia tarehe 11 – 13 Novemba 2016, Familia ya Mungu Barani Ulaya itaadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kwa watu wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi, hawa ni wale wanaoishi barabarani kama omba omba!

Maadhimisho haya yanafanyika Juma moja tu kabla ya kufunga rasmi maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu hapo tarehe 20 Novemba 2016, Mama Kanisa atakapofunga Malango ya Huruma ya Mungu kwa moyo wa shukrani kwa Fumbo la Utatu Mtakatifu, kwa kuliwezesha Kanisa kuadhimisha kipindi hiki cha neema, toba na wongofu wa ndani. Baba Mtakatifu anatamani kuona harufu nzuri ya huruma ya Mungu inawafikia wote pasi na ubaguzi, kwani huruma ni utambulisho wa Mungu! Kwa kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu watu hawa wataonja kwamba wanayo nafasi muhimu sana mbele ya macho ya Mungu na ni kiini cha maisha na utume wa Kanisa katika mchakato wa Uinjilishaji wa kina!

Tukio hili linaandaliwa na Chama cha Kitume cha “Fratello” “Udugu” kutoka Ufaransa, ambako mwaka huu pamoja na mambo mengine wanaadhimisha pia Mwaka wa huduma. Maskini na watu wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi watapata nafasi ya kusali, kutafakari na kuadhimisha matendo makuu ya Mungu katika maisha yao. Tarehe 11 Novemba 2016, Baba Mtakatifu Francisko atatoa katekesi na kilele cha maadhimisho haya ni Ibada ya Misa Takatifu itakaongozwa na Baba Mtakatifu hapo tarehe 13 Novemba 2016. Kipindi chote hiki ni muda wa shuhuda za maisha, sala na tafakari.

Kardinali Philippe Barbarin, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Lione ataongoza mkesha kwa ajili ya maadhimisho haya. Itakumbukwa kunako mwaka 2014, watu 150 wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi walibahatika kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko, na huo ukawa ni mwanzo wa Chama cha Fratello, “Udugu”. Vyama mbali mbali vya kitume kutoka Barani Ulaya vinavyojishughulisha kuwasaidia na kuwahudumia maskini na wale wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi vinahamasishwa kujiunga katika hija hii ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

Unaweza kuwasiliana nasi kwa kutumia e mail ifuatayo:

engafrica@vatiradio.va

Au kuandika barua kwa anuani ifuatayo:

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican,

Vatican Radio,

Vatican city, 00120.








All the contents on this site are copyrighted ©.