2016-05-03 12:15:00

Dhana ya usawa wa kijinsia inavyowavuruga watu!


Katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia kuna dhana ya “Usawa wa kijinsia” “Gender” inayoendelea kuchanganya na kuchafua akili za watu wengi, kwani huu ni mwelekeo ambao unataka kufutilia mbali tofauti za kijinsia kadiri ya mpango wa Mungu na kuona kila kitu ni sawa! Lakini ukweli wa mambo ni kwamba, jinsia hizi mbili ya kiume na ile ya kike, zimeumbwa na Mwenyezi Mungu ili ziliweze kukamilishana na wala si kwa bahati mbaya tu, kama wanavyodhani watetezi wa nadharia ya “jinsia” au “Gender”.

Kushindwa kutofautisha kati ya jinsia na kiume na ya kike ni dalili za kufilisika kabisa kwa binadamu kunakoonesha utupu wake katika sayansi na elimu ya binadamu. Hivi ndivyo Baba Mtakatifu Francisko anavyoandika kwenye Wosia wake wa kitume kuhusu “Furaha ya Upendo ndani ya familia, Namba, 56; tema ambayo imepembuliwa kwa kina na mapana hivi karibuni na Jukwaa la Wanawake Wakatoliki, huko Washington, DC. Marekani; kongamano lililoandaliwa na Kituo cha Maadili na Sera za Kijamii pamoja na Kituo cha Habari cha Kanisa Katoliki nchini Marekani.

Wajumbe wa kongamano hili la kimataifa ambalo mwaka huu limeingia awamu ya tatu, wameendelea kupembua jinsi ambavyo dhana ya “Jinsia” imeendelea kukua na kupanuka katika miaka ya hivi karibuni katika medani za kisiasa kitaifa na kimataifa; mwelekeo ambao una madhara makubwa katika mwono na mwelekeo sahihi kuhusu familia, utamaduni, taasisi na uhuru wa kidini.

Hotuba na majadiliano kati ya wajumbe yameonesha jinsi ambavyo mageuzi ya dhana ya “Jinsia” yanayoendelea kumong’onyoa tofauti za kijinsia, hatari kabisa katika kutangaza na kushuhudia Injili ya familia. Hivi ndivyo anavyofafanua Bi Ana Cristina Betancourt, Afisa kutoka Baraza la Kipapa la familia aliyeshiriki katika kongamano hili huko Washington, D.C. Marekani.

Kwa upande wake Mary Rice Hasson, Mkurugenzi wa Jukwaa la Wanawake Wakatoliki Marekani katika hotuba yake elekezi amegusia jinsi ambavyo Kanisa linapaswa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha Injili ya familia dhidi ya vitisho vinavyosababishwa na baadhi ya watu kutaka kukumbatia utamaduni wa kifo, hatari kwa maisha ya ndoa na familia. 

Mama Helen Alvarè, Rais wa Baraza la Ushauri la Jukwaa la Wanawake Wakatoliki nchini Marekani amewataka wajumbe kusimama imara kulinda, kutetea na kudumisha uhuru wa kidini unaotekelezwa na taasisi zinazoendeshwa na kusimamiwa na Kanisa Katoliki, kwani hapa zina kumbana na hatari ya kwenda kinyume kabisa cha utashi na dhamiri nyofu. Uhuru wa dhamiri unapaswa kuzingatiwa na wote.

Hii iwe ni sehemu ya mchakato wa Uinjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda wa maisha ya watu kwa kusoma alama za nyakati, tayari kutafuta lugha rahisi inayoeleweka kwa waamini wengi wakati kufundisha kweli za imani sanjari na kuwa na katekesi makini na endelevu! Waamini wasikubali kumezwa na malimwengu, bali wawe na ujasiri wa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha: utu, heshima, kanuni maadili na tunu msingi za maisha ya kiroho na kiutu!

Waamini wawe na ujasiri wa kukabiliana na changamoto za maisha kwa mwanga wa Injili ya huruma na upendo wa Mungu, dhana inayopewa kipaumbele cha pekee na Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Kwa namna ya pekee, binadamu anahamasishwa kulinda na kudumisha utu wake, kwa kujipokea, kujikubali na kujiendeleza kadiri ya mpango wa Mungu katika kazi ya uumbaji. Kutokana na changamoto ya “Jinsia” kuna haja kwa wazazi, walezi na wadau mbali mbali kuwa makini zaidi katika masuala ya elimu ya jinsia, ili kukubali na kuthamini tofauti za kijinsia kadiri ya mpango wa Mungu. Watu wawe na heshima ya kukubali miili yao kadiri walivyoumbwa na Mwenyezi Mungu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

Unaweza kuwasiliana nasi kwa kutumia e mail ifuatayo:

engafrica@vatiradio.va

Au kuandika barua kwa anuani ifuatayo:

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican,

Vatican Radio,

Vatican city, 00120.








All the contents on this site are copyrighted ©.