2016-05-03 10:14:00

Caritas Mbeya inapania kuwajengea wananchi uwezo wa kupambana na umaskini!


Idara ya Caritas na maendeleo Jimbo Katoliki la Mbeya,Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wafadhili kutoka ndani na nje ya nchi imekuwa ikijishughulisha na utume wa maendeleo ya jamii katika nyanja mbalimbali za maisha zikiwemo: kilimo, ufugaji, afya, elimu, uchumi na masuala ya utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote!

Askofu Evarist Chengula wa Jimbo Katoliki la Mbeya katika kuhakikisha kwamba Jimbo lake linamwendeleza na kumkomboa mwanadamu: kimwili na kiroho, kupitia Idara yake ya Caritas na maendeleo limefanikiwa kuunda vikundi hamsini (50) vya kuweka akiba na kukopa (SILC) kwa wanajamii wa Kata tisa za Wilaya ya Mbozi katika Mkoa mpya wa Songwe.

Mradi wa nafaka wa Shirika la CRS, Morogoro umekuwa ukisimamiwa na Idara ya Caritas na maendeleo Jimbo Katoliki la Mbeya na ndio unaoendesha mradi huo ambao kwa muda mfupi tangu mwezi  Juni, 2015 umewakutanisha pamoja wananchi zaidi ya 1,011 kutoka katika kata za Itaka, Magamba, Isansa, Bara, Itumpi, Igamba, Shiwinga, Nambinzo na Halungu, wilayani mbozi.

Bwana Andrea Mwaipopo ni Meneja wa Mradi wa nafaka kutoka Idara ya Caritas Mbeya, amezungumzia mwamko uliopo kwa wananchi na kwamba tayari kikundi cha Umoja cha kuweka akiba na kukopa kimefikisha miezi nane kwa mujibu wa katiba yao ya kuvunja kikundi na kugawana gawio ambapo zaidi ya akiba ya Sh.mil.4 wamegawana na kuanza utaratibu mpya wa kuweka na kukopa huku riba ikiwa ni asilimia nane tu ya fedha za kukopa ambapo hisa moja inauzwa kwa Sh.5,000.

Mkurugenzi wa Shirika la Caritas na Maendeleo Jimbo Katoliki la Mbeya, Edgar Mangasila amewawaasa wanavikundi vya kuweka akiba na kukopa(SILC) kuzitumia fedha za gawio kwa nidhamu kwa malengo ya kuwaletea maendeleo badala ya kuzifuja kwa mahitaji yasio muhimu ya anasa ikiwemo na kulewa ovyo pombe. Ameyasema hayo wakati wa hafla fupi ya wanakikundi cha Umoja katika kijiji cha Itewe,Kata ya Itaka,Wilaya ya Mbozi katika mkoa mpya wa Songwe huku akiwasihi wanakikundi hao na wengine wanaotumia utaratibu wa kujiwekea akiba na kukopa kuwekeza vizuri kwa malengo ya kujiinua kiuchumi huku akiwashauri kuacha kujinyima katika matumizi muhimu kwa manufaa ya familia.

Na Thompson Mpanji,Mbeya,Tanzania








All the contents on this site are copyrighted ©.