2016-05-02 06:49:00

Siku ya wafanyakazi duniani: Utu, heshima, usalama na ajira!


Mei Mosi ya kila Mwaka, Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha Siku kuu ya Wafanyakazi Duniani na Kanisa kwa upande wake linaadhimisha  kumbu kumbu ya Mtakatifu Yosefu, Mfanyakazi. Kanisa linatambua na kuthamini umuhimu wa kazi kama wajibu na utimilifu wa maisha ya mwanadamu sanjari na ushiriki wa mwanadamu katika kuitiisha dunia ili iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. Huu ni mwendelezo wa ushiriki wa mwanadamu katika kazi ya uumbaji na mchango katika kazi ya ukombozi.

Kumbu kumbu hii ilianzishwa na Papa Pio XII kunako mwaka 1955, Siku ambayo inaadhimishwa sanjari na Siku kuu ya wafanyakazi duniani, ili waweze kujifunza kutoka kwa Mtakatifu Yosefu, aliyesimama kidete kuitunza na kuitegemeza Familia Takatifu. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii kwa maadhimisho haya anaitaka Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inasimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu na heshima ya binadamu pamoja na usalama kazini.

Askofu mkuu Cesare Nosiglia wa Jimbo kuu la Torino, Italia anasema, familia ya Mungu Jimboni mwake, inaadhimisha Siku kuu ya wafanyakazi duniani kwa kukazia changamoto iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko mwaka mmoja uliopita alipotembelea Jimboni humo, anayekazia umuhimu wa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa: utu na heshima ya binadamu; utambulisho na ushiriki wake katika mchakato wa mafungamano ya kijamii. Anasema, ukosefu wa fursa za ajira una madhara makubwa katika utu na heshima ya binadamu, familia na jamii katika ujumla wake, kiasi kwamba, watu wengi wanakosa matumaini kwa leo na kesho iliyo bora zaidi.

Changamoto ni  kwa Serikali na sekta binafsi kuwekeza zaidi katika utengenezaji wa fursa za ajira hasa miongoni mwa vijana ili kufufua uchumi na kuwajengea watu matumaini, kwa kuwekeza katika majiundo makini na endelevu kwa vijana na wafanyakazi ili kuwapatia uwezo wa kutumia vyema karama na vipaji vyao kwa ustawi na maendeleo ya wengi.  

Kila mtu anapaswa kutekeleza dhamana na wajibu wake barabara, ili kusaidia mchakato wa maboresho ya uchumi na maisha ya watu! Jamii ijenge utamaduni wa majadiliano na upembuzi yakinifu; ushirikishwaji wa wengi na uwakilishi makini. Kanisa linatambua na kuthamini sana mchango wa wafanyakazi katika ustawi na maendeleo ya wengi, lakini linakazia umuhimu wa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu na heshima ya wafanyakazi, kwani kazi ni utimilifu wa utu na heshima ya binadamu! Anasema Askofu mkuu Cesare Nosiglia wa Jimbo kuu la Torino, Italia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.