2016-05-02 09:14:00

Mshikamano wa upendo na wananchi wa Ukraine!


Baba Mtakatifu Francisko kwa kuguswa na mateso pamoja na mahangaiko ya wananchi wa Ukraine kutokana na vita na mipasuko ya kijamii inayoendelea nchini humo, hivi karibuni aliwaalika waamini wa Kanisa Katoliki Barani Ulaya kuchangia kwa hali na mali, ili kuwasaidia wananchi wa Ukraine wakati huu mgumu wa historia ya maisha yao. Fedha hiyo tayari imekwisha kusanywa na Monsinyo Giampiero Dal Toso, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa linaloratibu misaada ya Kanisa Katoliki, Cor Unum amerejea kutoka Kiev na kusema kwamba, tayari Kanisa limeunda kamati maalum ya kusimamia na kuratibu mfuko huu maalum kwa ajili ya kuwasaidia wananchi wa Ukraine kadiri ya utashi wa Baba Mtakatifu Francisko.

Monsinyo Dal Toso anasema, Kanisa linapenda kuwasaidia wananchi kutokana na madhara ya vita na myumbo wa uchumi, hali ambayo imepelekea huduma za afya, elimu na ustawi wa jamii kuzorota kwa kiasi kikubwa. Msaada huu katika awamu ya kwanza utasaidia kutoa chakula cha dharura, makazi, dawa na mavazi hasa kwa watoto na wanawake wanaokabiliwa na hali ngumu zaidi.

Msaada huu unatolewa kwa wananchi wote pasi na ubaguzi na kwamba, mradi huu umepata pia mwitikio wa kiekumene unaojikita katika huduma ya mapendo kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Viongozi wa Kanisa Katoliki watashirikiana na viongozi wa Kanisa la Kiorthodox ili kuwahudumia wahitaji zaidi.

Viongozi wa Serikali ya Ukraine wanamshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa kuguswa na mahangaiko ya maskini na kuamua kutenda kwa hekima na busara, kama sehemu ya mchakato wa kumwilisha Injili ya huruma na mapendo, hasa mwaka huu Kanisa linapoadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Tarehe 24 Aprili 2016, ilikuwa ni siku maalum ya kuchangia wananchi wa Ukraine, ikawa pia ni fursa ya kuzungumza kuhusu vita ambayo inaonekana kusahauliwa na Jumuiya ya Kimataifa, lakini kuna mamillioni ya watu wanaoendelea kuteseka kwa vita na mipasuko ya kijamii na kisiasa.

Imekuwa ni fursa ya kuragibisha mateso na mahangaiko ya wananchi wa Ukraine Barani Ulaya! Monsinyo Dal Toso akiwa nchini Ukraine, ametembelea kambi ya wakimbizi na kujionea mwenyewe mateso na mahangaiko ya wananchi. Hawa ni watu waliokuwa wanaishi maisha ya kawaida kwenye makazi yao, lakini kutokana na vita kwa sasa wanalazimika kuishi kwenye kambi za wakimbizi. Ni watu ambao hawana tena matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi. Kanisa linaendelea kushikamana na wananchi wa Ukraine wanaoteseka kutokana na vita ambayo inaonekana kusahauliwa hata na wananchi wa Umoja wa Ulaya!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.